January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waraka wa Dk. Chami umesheheni upotoshaji

Mbunge wa Moshi Vijijini CCM, Dk. Cyril Chami

Spread the love

MBUNGE wa Moshi Vijijini (CCM), ametoa andishi alilolituma kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), akilalamikia madhehebu ya Kikristo kukosoa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.

Waraka wa madhehebu ya Kikristo umetolewa kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania (CCT). Umesambazwa kwenye makanisa yote nchini kwa lengo la kuelemisha waamuni wake umuhimu wa Bunge la Katiba, kuheshimu maoni ya wananchi.

CCT imesema, “Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma limekosa uhalali.”

Katika waraka wake, Dk. Chami anasema, ameandika kwa niaba ya wabunge wenzake ambao ni waumini wa Jumuiya ya Mtakatifu Thomas More, iliyoko mkoani Dodoma.

Ukisoma andishi la Dk. Chami, tangu mwanzo anaonyesha kila kisichokuwa cha Kanisa Katoliki, hakifai.

Kwa mfano, Dk. Chami anasema, yeye na wenzake walipouona waraka huo hawakutilia maanani kwa sababu haukuwa na sahihi na wakatatoliki na wala haukutumia mfumo wa kichungaji wa kikatoliki.

Tatizo la Dk. Chami, siyo waraka kukosa sahihi. Tatizo ni kukosekana kwa sahihi ya mkatoliki. Unaweza ukaweka sahihi, lakini kama aliyeweka sahihi siyo mkatoliki, yeye hautambui.

Hakika, andishi la Dk. Chami, limesheheni upotoshaji. Limesheheni itiikadi na limelenga kuangamiza taifa. Sababu ni zifuatazo:

Kwanza, Dk. Chami anadai umakini wa Kanisa Katoliki unatokana na wingi wa waumini wake. Anasema kanisa hilo limekuwa kitu kimoja kwa muda mrefu; jambo ambalo linasababisha madhehebu mengine kuwaonea wivu. Siyo kweli.

Umakini wa kanisa Katoliki hautokani na wingi wa waumini iliyonao. Mafundisho ya kanisa hili ni yale yale duniani kote; iwe katika nchi ambamo wakatoliki ni wachache sana au wengi.

Pamoja na wingi wake na historia kanisa kuwa kama mama ulimwenguni, bado kanisa Katoliki linatambua uwepo wa madhehebu mengine na inayaheshimu.

Kudai umakini wa Kanisa Katoliki unatokana na wingi wa wafuasi wake, ni kutaka kulidhalilisha. Kuna taasisi nyingi zenye wafuasi wengi, lakini siyo makini.

Viongozi wa madhehebu ya Kikatoli wamesaini waraka wa jukwaa, kwa sababu ya umakini wake; siyo wingi wa waumini wake.

Hatua ya Dk. Chami kuibuka na kujifanya muumini mzuri kuliko Baba Mtakatifu Papa Fransis, siyo kigezo cha kulifanya kanisa lote lisitambue uwepo wa makanisa mengine.

Pili, Dk. Chami anasema Waraka wa CCT unawagawa wakristo ndani ya Bunge la Katiba; wakatoliki walioko Bunge la Katiba, wanawakilisha maslahi ya kanisa Katoliki.

Anasisitiza, “waraka wa Jukwaa la Wakristo haukusomwa katika makanisa mengine yasiyo ya Kikatoliki.”

Ni muhimu muandishi wa waraka (Dk. Chami), akaelewa kuwa wabunge ambao ni waumini wa madhehebu ya Kikatoliki na wengine, hawakuingia bungeni kwa ajili ya ukatoliki wao na wala hawako bungeni kuwakilisha maslahi ya kanisa Katoliki.

Waraka wa Jukwaa la wakristo ni sauti wakristo wote – wanachama wa jukwaa hilo. Waraka umelenga kuunganisha waamini wake ili washiriki kikamilifu katika kupata katiba bora.

Kinachomsumbua Dk. Chami, amejikuta yuko njia panda. Anashindwa kujigawa – afuate ushauri wa viongozi wa dini au shinikizo la chama chake.

Aidha, waraka kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, umesomwa na bado unasomwa katika makanisa yote wanachama wa jukwaa hilo. Katika baadhi ya maeneo, waraka huu unauzwa hadi Sh. 1, 000 (shilingi elfu moja).

Tatizo analopata Dk. Chami, katika maisha yake hajawahi kukanyaga katika makanisa mengine, nje ya kanisa katoliki. Yeye anaamini nje ya Kanisa Katoliki, hakuna makanisa mengine.

Ni muhimu atumie dhana hii ili atangazwe mwenye heri atakapokufa; lakini asilazimishe imani yake katika masuala ya siasa.

Tatu, Dk. Chami anadai kanisa Katoliki na CCM, ni kitu kimoja; wanachama wa chama hicho watakapothibitisha kuwa “badala ya Kanisa lao kuwatumia kujijenga zaidi, limetumia nguvu yake kukibomoa chama chao cha siasa.”

Huku ni kudhalilisha chama hicho na kulitusi kanisa. Kanisa Katoliki ni kwa ajili waumini wake na haliwezi kuchanganywa na mifumo ya kiitikadi. Kanisa haliwezi kuenea ndani ya CCM na wala CCM haiwezi na haina haja ya ukatoliki ili kutekeleza ilani yake.

Vinginevyo, kwa kuwa Dk. Chami ni muumini wa madhehebu ya Kikatoliki na mwanachama wa CCM, basi atakuwa anafahamu mengi zaidi kati ya kanisa na chama chake.

Nne, Dk. Chami anafananisha uchaguzi ndani ya chama chake na uchaguzi wa Papa. Hii ni kufuru. Dk. Chami anapaswa kufungiwa sakramenti na kurudishwa darasa la kipaimara. Hakuna anayeweza  kufanananisha uchaguzi wa Papa na uchaguzi wa CCM. Baba Mtakatifu (Papa), huchaguliwa na Baraza Maalum la Makardinali. Kura zake hazitangazwi. Ikiwa Papa anachaguliwa kwa wingi wa kura au uchache wa kura, ni kanisa pekee linalojua.

Lakini Dk. Chami anadai kwa kuwa Papa huchaguliwa kwa wingi wa kura, basi Kanisa Katoliki na viongozi wake hawana haki ya kuhoji wingi wa wabunge wa CCM kwa sababu wamechaguliwa kwa wingi wa kura kama anavyochaguliwa Papa!

Hakuna asiyejua jinsi Dk. Chami na wabunge wenzake walivyoingia bungeni. Hata udhaifu wa kufanya maamuzi unatokana na jinsi walivyotangazwa kuwa washindi kwa “kura nyingi.”

Tano, anatuhumu Serikali ya Zanzibar na Wazanzibari kwa jumla, kuwa wameridhia mauaji ya mapadri. Anasema kuruhusu serikali tatu kutaifanya Zanzibar kujitangaza taifa la Kiislamu na hivyo mapadri kuendelea kuchinjwa.

Amelenga kuaminisha umma kuwa Muungano umekuja ili kudhibiti uislam nchini na hasa Zanzibar.

Ni kweli Mapadri wameshambuliwa Zanzibar. Wengine wameachwa vilema. Lakini hayo yametokea hadi Arusha ambako Balozi wa Papa alinusurika kifo.

Wala vitendo hivi havikufanyika kwa sababu ya uislamu. Vimefanyika kwa udhaifu wa dola isiyosimamiwa na chama chake. Suala la Wazanzibari kuridhia mauaji hayo, lingejulikana kama dola ingekuwa imara.

Udhaifu wa dola usiwe kigezo cha kuwasingizia raia wa Visiwani kama Dk. Chami anavyotaka kuaminisha.

Dk. Chami anaandika kuwa jamii ya walio wengi Zanzibar imeyakubali mauaji. Mko wapi mlio wengi kwenye serikali ili mpambane na walio wengi wanaowachinja kama kuku mapadr?

AnasemaTanzania Bara wanashirikiana na majeshi kuwakamata wauaji. Yaani nchi ile ile, jeshi lile lile, watu wale wale, wanaopendwa kwa wingi wamechaguliwa na wako madarakani, bado anasema, “wao wa Bara wana ushirikiano, wale wa Zanzibar hawana ushirikiano? Hiyo kweli ni nchi moja?

Hata hivyo, sisi wa Bara anatusifia kwa ushikirikiano upi? Mabomu kule Arusha na kwingineko, tumetoa ushirikiano na wahusika wakakamatwa? Huyu anawataka Al-Gaeda au Al-Shabaab wanaoua kwa njia ipi?

Kama Mapadri wamechinjwa kama kuku Zanzibar (kwa maneno yake); anachotaka kuona ni nini zaidi?

Anasema, “… tuko karibu mno na Zanzibar.” Nani anajali umbali alipo adui yake? Anataka kutwambia kuwa Marekani iko karibu sana na Afganistan, na kwamba ndicho kilichomsaidia Osam bin Laden kuishambulia?

Maneno haya yaliyomo katika andishi la Dk. Chami yanatisha. Madhumuni ya Muungano, siyo kulinda ukiristo. Wala ukristo haulindwi na muundo wowote wa Muungano. Kuna sehemu nyingi hakuna Muungano, lakini ukristo upo.

Ikiwa Zanzibar huru itaamua kuanzisha dola ya kiislamu, isiwe hoja ya kuchonganisha kanisa na serikali.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, “watu waliofilisika kisiasa hukimbilia kujificha ndani ya ukabila na udini.” Yawezekana Dk. Chami, ni miongoni mwa waliofilisika.

Ikiwa andishi la Dk. Chami ndiyo msimamo wa chama chake,  inahitajika hekima na uthubutu wa haraka kuunyamazisha waraka huu ili kunusu taifa lisitumbukie katika machafuko.

error: Content is protected !!