Wednesday , 29 March 2023
Home Kitengo Maisha Elimu Waraka maalumu kwa NECTA, “hawapaswi kuungwa mkono”
ElimuMakala & Uchambuzi

Waraka maalumu kwa NECTA, “hawapaswi kuungwa mkono”

Spread the love

HATUA iliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), ya kufuta utaratibu wa kutangaza shule bora na wanafunzi bora katika matokeo ya mitihani ya taifa, ni hatua isiyopaswa kuungwa mkono hata kidogo kutokana na sababu zifuatazo;

Mosi; Ushindani ni muhimu sana katika elimu. Ushindani huchochea hamasa, bidii na wajibu wa kufanya vizuri zaidi.NECTA hawakupaswa kufuta kabisa ushindani, bali walipaswa kuboresha mazingira, vigezo na viwango vya ushindani baina ya shule na shule, na baina ya wanafunzi na wanafunzi.

Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Salumu

Pili; Kama hoja yao ilikuwa ni kuepuka  kushindanisha shule na wanafunzi kwasababu ya kusoma katika mazingira tofauti kama walivyoeleza; basi kilichopaswa kufanywa na NECTA ni kuyapanga matokeo ya shule hizo katika makundi tofauti tofauti ya shule zinazofanana, na kisha kuzitangaza shule bora zilizofanya vizuri zaidi kulinganisha na nyiñgine kwenye kundi husika. Na wangeweza pia kutangaza wanafunzi bora kwa kufuata utaratibu huo huo, ili kuchochea ushindani na wajibu wa kuchukua hatua za kuongeza ubora wa elimu.

Mathalan, shule za binafsi zingeweza kupimwa kwenye kundi lake, na shule za serikali zingeweza kugawanywa katika makundi kadhaa kulingana na mfanano wa mazingira yao. Mfano sekondari za kata, zingeweza kushindanishwa kwenye kundi lao; kwa hiyo,  tatizo la kushindanisha shule zisizoendana lingekuwa limetatuliwa lakini utaratibu wa ushindani ungebaki palepale.

Tatu; Kwa kukiri kuwa shule zina mazingira tofauti ya elimu na kwa hiyo hazipaswi  kushindanishwa kwa pamoja, serikali inakuwa ni kama imeridhika na utaratibu wa baadhi ya wanafunzi kufundishwa kwenye shule zenye mazingira bora na wengine kusoma kwenye shule zenye mazingira duni. Hii ni sawa na serikali kukiri uwepo wa matabaka na kukubali kuyakumbatia matabaka hayo katika elimu. Hiyo si sawa.

Kwa kuzingatia mikataba mbalimbali ya kimataifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuhusu umuhimu wa kuondoa utofautiano katika elimu na kuhakikisha kunakuwa na usawa na mifumo jumuishi katika elimu, Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha shule zote zinaboreshwa na kuhakikisha matabaka katika elimu yanapunguzwa na kuondolewa kabisa, ili kuwahakikishia watoto wote wa kitanzania haki sawa na fursa sawa ya kupata elimu iliyo bora.

Nne; Kwa upande mwingine, ni dhahiri kuwa hatua ya NECTA, imelenga kuficha aibu ya shule nyingi za serikali hususan sekondari za kata ambazo zimekuwa hazifanyi vizuri kulinganisha na shule binafsi. Serikali inapaswa kuchukua hatua za kuboresha mazingira na ubora wa elimu inayotolewa kwenye shule zake zote za msingi, sekondari na vyuo badala ya kuweka “mpira kwapani” kwa kukimbia changamoto za kiushindani ambazo zimekuwa zikitolewa na shule binafsi.

HALI HALISI YA ELIMU

Tano; Pamoja na ujenzi wa shule na madarasa unaoendelea maeneo mbalimbali nchini, hususan kwa kutumia fedha za mikopo iliyotolewa kupitia Mpango wa kukabiliana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19; bado hali ya elimu nchini, kwa shule za msingi na sekondari, ni mbaya kwasababu ya mazingira duni ya shule, maslahi duni ya walimu na mfumo wenyewe wa elimu pamoja na mitaala yake kushindwa kuzalisha wasomi wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Edward Kinabo

Sita; Mathalan, pamoja na ujenzi wa madarasa, leo watoto wengi wa shule za msingi katika mji wa Mlandizi, wilaya ya Kibaha, wanakaa chini kwenye vumbi, kwasababu ya uhaba mkubwa wa madawati. Tatizo hilo ni kubwa kwa karibu kwa shule zote za Mlandizi, hususan katika shule ya msingi Mtongani, iliyopo ndani ya Mji Mdogo wa Mlandizi, wilaya ya Kibaha, mkoa wa Pwani. Ushahidi wa picha zilizopigwa hivi karibuni na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jimbo la Kibaha Vijijini, unathibitisha jinsi watoto wengi wanavyokalishwa chini kwasababu ya uhaba wa madawati. Hali hiyo inaathiri ubora wa elimu na kusababisha wanafunzi hasa wa shule za serikali kufanya vibaya katika mitihani yao ukilinganisha na wale wa shule za binafsi.

Saba; Ni vema ikazingatiwa kuwa tatizo la msingi zaidi la elimu yetu, si ufaulu mdogo wala mkubwa, bali ni elimu duni isiyokidhi mahitaji ya ujuzi na umahiri unaohitajika katika soko la ajira nchini na dunia nzima kwa ujumla*

Nane; Ukweli huu unathibitishwa na Ripoti ya Utafiti wa UNICEF, Commission for Education, iliyozinduliwa katika siku ya ujuzi kwa vijana duniani mwaka jana World Youth Skills Day 2022). Kwa mujibu wa ripoti hiyo, 75% ya vijana wa Kitanzania hawana ujuzi wala umahiri unaohitajika katika ajira. Pia, 62% ya watoto wa umri wa miaka 10 Tanzania (wa elimu ya msingi) hawawezi kusoma vizuri hata sentensi fupi ya kawaida na 83% hawamudu kuhesabu vizuri tarakimu. Kwa ujumla, ripoti hii (ya hivi karibuni kabisa) imeweka bayana kuwa wanafunzi nchini Tanzania hawapati msingi mzuri wa elimu wala kujengwa katika ujuzi/stadi muhimu utakaowapa fursa ya kuja kuajirika au kujiajiri*

Tisa; Pia, ukweli huu umethibitishwa pia na ripoti na taarifa mbalimbali za Shirika la Kazi Duniani (ILO), World Bank na UNDP kuhusu kuwepo kwa changamoto kubwa ya pengo la ujuzi katika kundi kubwa la vijana wa Kitanzania, takribani 900,000 wanaoingia kwenye soko la kufukuzia ajira kila mwaka.

HATUA ZINAZOPASWA KUCHUKULIWA

Mosi; Ili kuboresha mazingira ya shule za serikali, ninaishauri  Serikali kuu, hususan, kupitia TAMISEMI na Wizara ya Elimu, ziingilie kati kwa haraka na kutatua tatizo kubwa la madawati lililopo kwenye maene mbalimbali nchini, hususan katika Mji Mdogo wa Mlandizi na wilaya nzima ya Kibaha, ambako tayari  kumethibitika kuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa madawati madawati.

Aidha, ninatoa wito na kuwaomba wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda mbalimbali vilivyomo ndani na nje ya Jimbo la Kibaha Vijijini na wilaya ya Kibaha, pamoja na watu wengine wote wanaoguswa na elimu, wajitokeze kwa wingi katika kuisaidia serikali kutatua tatizo kubwa la dharula ya madawati, kwa kuchangia madawati kupitia shule husika zinazokabiliwa na changamoto hiyo, kwa haraka iwezekanavyo ili watoto wetu wasiendelee kukaa kwenye vumbi.

Pili; Serikali ijiandae kuingiza kwenye bajeti ya elimu mahitaji yote ya kuwezesha kutoa huduma ya lazima na ya uhakika ya chakula cha mchana kwa wanafunzi mashuleni, badala ya kuachia jambo hilo wadau kama jambo la hiyari au khisani tu.

Aidha, wadau wa elimu na maendeleo, wakiwemo wafanyabiashara, viwanda na makampuni mbalimbali yaliyopo nchini, nayahamasisha kujiwekea utaratibu wa kuchangia nafaka, mafuta na vyakula mbalimbali mashuleni ili kuchochea mazingira bora ya elimu shuleni.

Tatu; Serikali iongeze uwazi na ushirikishwaji wa wadau katika mchakato unaoendelea wa kupokea  na kuchakata maoni kwaajili ya kufanya mageuzi ya mitaala, mfumo wa udhibiti ubora wa elimu, maslahi ya walimu pamoja na motisha, ili Sera, mipango ya elimu pamoja na bajeti za sekta ya elimu, vizingatie haja ya kuzalisha wasomi wenye ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Nne; Serikali ihakikishe kuwa suala la kuongeza mishahara, na kutoa motisha kwa walimu, linàkuwa ndiyo kipaumbele namba moja katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini.

Uchambuzi huu umeandaliwa na Edward Kinabo – Mwanaharakati wa Maendeleo pia alikuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & Uchambuzi

Ujio wa Kamala Harris: Fahamu uhusiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani

Spread the love  TANZANIA ni miongoni mwa nchi tatu ambazo zimebahatika kutembelewa...

ElimuHabari

Serikali yataka vijana  wajiunge na program atamizi ya biashara CBE

Spread the love  SERIKALI imewahamasisha vijana kujiunga na program atamizi inayotolewa na...

Makala & Uchambuzi

ZITTO: Hii ndio sababu Malaysia kuushinda umasikini kupitia kilimo, Tanzania ikikwama

Spread the love  MNAMO Februari 2017, miaka sita sasa imepita, niliandika, kupitia...

Elimu

Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini wamwaga mamilioni ujenzi maabara za sekondari

Spread the love  MFUKO wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara,...

error: Content is protected !!