Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wapinzani washangaa wabunge CCM kujipendekeza kwa Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Wapinzani washangaa wabunge CCM kujipendekeza kwa Magufuli

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo
Spread the love

KASI ya “kujipendekeza” ya baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli, imeshangaza waengi, wakiwamo viongozi wa upinzani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, leo Jumatano, tarehe 10 Februari 2021, katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema, walioanzisha mjadala huo, ni watu wasiojiamini.

Amesema, “hawa watu wanaotaka Rais Magufuli aongezewe muda wa kubaki madarakani, hawana uhakika wa kuchaguliwa tena na wananchi kurudi bungeni.”

Anasema, “ukiona wabunge wanaacha ajenda za wananchi na kushabikia mambo ya kumuongezea rais muda, basi fahamu kuwa wanadhani ubunge wao, uko mikononi mwa rais na si kwa wananchi.

“Naamini mjadala ulioanza kwenye Bunge kutaka rais aongezewe muda wa kukaa madarakani, ni maneno ya watu ambao hawana hoja zinazoendana na kinachojadiliwa bungeni. Wanataka kujipendekeza kwa rais, ili waonwe na wakumbukwe katika ufalme wake.”

Mjadala wa kutaka Rais Magufuli aongozewe muhula wake wa urais, ulipamba moto bungeni wiki iliyopita, baada ya baadhi ya wabunge wakiongozwa na mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga, kudai kuwa ni sharti rais huyo aongozewe muda, ili kukamilisha kazi alizozianza.

Mwingine aliyekoleza hoja hiyo, ni mbunge wa Geita Vijijini (CC), Josephat Msukuma.

Naye naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya amesema, walioanzisha mjadala huo, wanajipendekeza ili wapate fursa serikalini.

Amesema, “nasema kwamba Bunge ni taasisi, yale ni maoni yake na uzuri kuongea hakuna kulipa kodi, ingekuwa kuongea kunalipa kodi, mtu ungekuwa unaongea kile kitu kinacholeta tija kwa taifa.

“Yawezekana wanajua kuwa labda Rais Magufuli akiwepo, kuna kamrija fulani wamekitegesha mahali kitaendelea kunyonya.”

Joseph Msukuma, Mbunge wa Geita Vijijini

Sakaya amesema, suala la kuongezewa muda rais halina afya kwa taifa, kwa kuwa litakwenda kinyume na misingi ya Katiba na utamaduni tuliyojiwekea, kwamba Rais ataongoza kwa vipindi visivyozidi viwili vya miaka mitano mitano.

“Waliounda Katiba na kuweka miaka 10 walikuwa na uelewa wa kutosha, walituwekea msingi imara,” amesema Sakaya na kuongeza “kwa miaka 10 kama kweli mtu unaongoza kwa kutumia akili, uwezo na utashi utakuwa umechoka. Huna jipya, inabidi upishe wengine waendelee.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye, amemshauri Rais Magufuli kutoingia kwenye mtego huo wa kukubali kuongezewa muda wa kukaa madarakani.

“Rais Magufuli akimalizia muda wake, apumzike na yeye tunamshauri asije kuingia kwenye huu mtego. Kama rais anafanya mazuri, anaweza kufanya mazuri akiwa nje kwa kumshauri aliyeko madarakani.

Edward Sembeye, Mkuu wa Mawasiliano ya Umma NCCR-Mageuzi

“Tamaduni ya taifa letu unaongoza kwa miaka 5, unachaguliwa tena, tofauti na hapo inakuwa kinyume na utaratibu tuliojiwekea,” amesema Simbeye.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe amesema, suala hilo limeibuliwa na watu wenye masilahi yao binafsi.

“Ni wapuuzi tu, nasema ni wapuuzi, hawaeleweki wanachosema ni nini. Ni matakwa ya nafsi zao, wanataka maisha yao yaende sawa, kwa ajili ya masilahi yao. Sio kwa ajili ya rais,” amesema Rungwe.

Katibu Mkuu wa Chama cha Democraticy Party (DP) Abdul Mluya amesema, wabunge hao hawatafanikiwa kwa kuwa Rais Magufuli haoineshi dalili za kutaka kuendelea kukaa madarakani.

“Hili jambo la rais kuongezewa muda, nafikiri ameshalijibu kabla ya uchaguzi mkuu. Amesema, anaheshimu Katiba na naamini anaheshimu kabisa, na hivyo hawezi kubariki jambo hilo.

“Mpaka sasa, hatujaona element (vishiria) za yeye kutaka kujiongezea muda. Nadhani haya mambo yanafanywa na wapambe tu,” ameeleza Mluya.

Kauli ya Mluya inaungwa mkono na kile kilichoelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, jana Jumanne tarehe 9 Februari 2021, bungeni mjini Dodoma.

Polepole ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na Rais Magufuli amesema, kiongozi huyo, hayupo tayari kubadili Katiba ili kusalia madarakani.

1 Comment

  • Asante ndugu shaibu lakini uwelewe kueleza sifa njema za matendo mema kwa binadamu mwenzio ni jambo jema na wala sio kujipenkeza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!