March 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wapinzani waliohamia CCM, wapewa ‘ofa’ maalum na Serikali

Naibu Waziri Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Josephat Kandege. Picha ndogo, Marwa Chacha, Mbunge wa Serengeti (CCM)

Spread the love

BAADHI ya mawaziri wamewapongeza wabunge waliohamia CCM wakitokea vyama vya upinzani, wakisema kuwa wana uhakika na kile walichokiamua katika kuungana na timu ya ushindi. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akijibu swali la Mbunge wa Serengeti, Marwa Lyoba Chacha, Naibu Waziri Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Josephat Kandege amesema muungwana anayekuzawadia zawadi, inapaswa kumjibu kwa uungwana, huku akimuahidi kutekeleza ombi lake la ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa km 4 katika mji wa Mgumu, katika mwaka wa fedha ujao.

“Naomba kwa dhati kabisa nami niungane na wabunge waliojiunga na timu ya ushindi, wana uhakika wanachokiamua, nimuhakikishie kupitia TARULA tutahakikisha tunatenga fedha.Kwa muungwana anayekuzawadia zawadi hii inapaswa kujibu kwa uungwana,” amesema Kandege.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi aliyehamia CCM akitokea Chadema, amempongeza mbunge huyo kwa kujiunga na timu ya ushindi kwa ajili ya kuletea maendeleo wapiga kura wake.

Katika swali lake, Mkundi alisema ilipotokea ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere tarehe 20 Septemba 2018 katika kisiwa cha Ukara, ilionekana changamoto ya ukosefu wa vifaa na magari ya kubebea wagonjwa, na kuhoji serikali ina mpango gani katika kutoa gari kwenye kituo cha afya cha Bwisya.

Ambapo Ummy alimhakikishia Mkundi kwamba, serikali ina mpango wa kununua magari 70 hivi karibuni na kwamba yatakaponunuliwa, gari moja litapelekwa jimboni kwake Ukerewe.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mwita Waitara aliyehamia CCM akitokea Chadema, wakati akijibu swali la Mbunge wa Simanjiro, James Ole Milya, alimpongeza kwa hatua yake ya kurudi CCM akisema kuwa amerudi mahali pake.

error: Content is protected !!