September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wapinzani wamng’ang’ania Rais Magufuli mezani

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Spread the love

CHAMA cha NCCR Mageuzi kimeiomba serikali kuweka meza ya maridhiano na vyama vya upinzani, ili kuzungumzia changamoto zinazoikabili demokrasia hapa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Wito huo umetolewa na James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi leo tarehe 27 Julai 2019 wakati akihutubia katika mkutano mkuu wa chama hicho, uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Mbatia amesema upinzani siyo uadui na kwamba ni vyema tofauti zilizopo katika uwanja wa siasa zikaondolewa, ili haki itendeke na kuienzi amani ya nchi kwa maendeleo ya Watanzania wote.

“Tunasema upinzani siyo uadui lazima tukubaliane, mabadiliko yote yanaanza katika mabadiliko ya fikra. Hakuna mtu mwenye hati miliki ya fikra. Ndiyo maana tuliandika kitabu upinzani siyo uadui, na upinzani ni kubadilishana fikra, kwamba wewe unataka kufanya hili mimi nataka liboreshwe hili,” amesema Mbatia.

Mbatia amesema siyo lazima vyama vya upinzani vilalamike kuhusu changamoto vinavyokabiliana navyo, kwa kuwa mamlaka husika, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inaona mwenendo wa hali ya siasa nchini, ikiwemo baadhi ya vyama kunyimwa fursa ya kufanya mikutano.

“Huwezi kusema chama A kina haki zaidi kuliko chama B, mwengine akifanya mkutano wa ndani inakua shida mwingine ana haki kufanya mkutano wa ndani. Naibu msajili wa vyama sijalalamika, sio lazima kila kitu tulalamike mnayaona. nchi hii si yetu sote,” amesema Mbatia na kuongeza.

“Haki ikizingatiwa na mimi niko tayari tuyazungumze katika meza ya maridhiano ya kuleta fikra zetu pamoja, ili haki ikitendeka tutapata amani, ikipatikana inakua nguzo sahihi ya kuwa na mifumo imara na endelevu, kwa taifa zima.”

Kuhusu mkutano mkuu wa leo, chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa, ili kupanga safu yake ya uongozi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mbatia amesema atafurahi kuona kwamba wajumbe wa mkutano huo watachagua mwenyekiti wa kike, ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya haki sawa kwa jinsia zote.

“Sijazaliwa niwe mwenyekiti wa kudumu wa NCCR Mageuzi, chama hiki kingepata mwenyekiti wa kike ingekuwa vizuri, ili yale tunayoyahubiri tuhubiri kwa vitendo,” amesema Mbatia.

error: Content is protected !!