November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wapinzani kutinga Ikulu, Mbowe atuma ujumbe kwa JPM

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

ZIARA za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani kuteta na Rais John Magufuli  Ikulu jijini Dar es Salaam,  zimemuibua Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe ameibuka na kuweka wazi kwamba, Chadema haiungi mkono mazungumzo yaliyofanywa na viongozi hao, na kumtaka Rais Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vyote kwa pamoja, kwa ajili ya kujadili mustakabali wa taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kiongozi huyo wa Chadema ametoa msimamo huo jana tarehe 8 Machi 2020, wakati akizungumza katika Sherehe ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanywa na Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), jijini Dar es Salaam.

 Wakati huo huo, Mbowe ameoneshwa kushangazwa na kitendo cha Rais Magufuli kutojibu barua ya Chadema, aliyoandikiwa hivi karibuni kuhusu mapendekezo ya upatikanaji wa uchaguzi huru na wa haki na kuamua kuwaita kimya kimya baadhi ya viongozi wa upinzani.

“Mimi nataka nitoe msimamo wa Chadema, kwanza wako wengi walihoji Mbowe hakupenda kwenda? Napenda kusema sikualikwa, lakini hoja si kualikwa, hoja ni kualikwa kwa utaratibu gani na tukafanye nini?

Sisi tumemuandikia rais barua tukimueleza kuna mambo matatu ya msingi kujenga taifa lenye umoja. Lakini rais hajajibu barua yetu,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema Rais Magufuli anatakiwa kujibu barua ya Chadema kwa kuhakikisha kwamba mapendekezo yaliyomo kwenye barua hiyo yanafanyiwa kazi, badala ya kueleza kwa maneno kwamba uchaguzi mkuu ujao utakua huru na wa haki.

Amesema Rais Magufuli anatakiwa kukutana kwa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa vyote, asasi za kiraia na wadau wote katika masuala ya uchaguzi, badala ya kualika watu wachache.

“Watu wananiambia mbona sijaenda Ikulu, siwezi kwenda Ikulu kutafuta uchumba, siwezi kwenda peke yangu akitaka atualike sisi kama Chadema taasisi, rais awe na wa kwake tuzungumze maisha ya wananchi. Rais atambue mbali na Chadema, kuna taasisi nyingi zenye maumivu,” ameeleza Mbowe na kuongeza:

“Sasa maneno ya uchaguzi kuwa huru wakati vyombo vyote viko upande mmoja, tunakuambia rais sio ukweli. Tunamwambia rais uchaguzi kuwa wa haki si kwa kauli zake. Tufanye marekebisho ya sheria katika bunge litakaloanza hivi karibuni.”

Hivi karibuni Rais Magufuli alifanya mazungumzo katika nyakati tofauti na baadhi ya viongozi wa vyama upinzani nchini, akiwemo Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, na Maalim Seif Sharrif Hamad, Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Viongozi hao wa upinzani baada ya mazungumzo yao na Rais Magufuli, walieleza kwamba, kiongozi huyo wa nchi amewahakikishia kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa huru na wa haki.

error: Content is protected !!