July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wapewa muda kubomoa vibanda vyao Dodoma

Spread the love

KAIMU Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Mjini, Clement Mkusa, ametoa siku 30 kwa Wafanyabiashara zaidi ya 100 wa Soko Kuu Majengo kubomoa vibanda vyao vilivyojengwa pembezoni mwa Mto Pombe. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mkurugenzi, huyo, amesema lengo la kuwaondoa wafanyabiashara hao ni kwa ajili kuimarisha hali ya usafi katika mto huo ili kuepuka maradhi ya milipuko ikiwemo kipindupindu.

Akizungumza na wandishi wa habari mjini hapa, Mkusa, alisema wafanyabiashara hao wanapaswa kubomoa vibanda hivyo, kwa vile hadi sasa hawana mkataba unaowapa uhalali kuendelea kuepo katika eneo hilo.

Alisema utekelezaji wa agizo hilo umeanza Desemba 8, mwaka huu baada ya mkurugenzi huyo kukabidhi barua za kuwataka wafanyabiashara hao kuondoka ndani ya siku hizo.

“Tumewakabidhi barua zao na wamezipokea tunacho subiri ni utekelezaji, pia naamini kuwa watatii agizo hilo, kwa sababu halikutolewa na Manispaa bali limetoka ngazi ya juu, “alisema Mkusa.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara katika Soko hilo, Godson Lugozama, alisema endapo Manispaa hiyo itaendelea kushikilia misimamo wake wa kubomoa vibanda 100 hivyo, basi wataendesha mgomo wakusitisha kutoa huduma sokoni hapo kwa muda usiyojulikana.

Lugozama, alitoa kauli hiyo mbele ya Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Clement Mkusa, wakati alipofanya ziara sokoni hapo kwa ajili ya kuwajulisha mpango huo.

Aliwataja wafanyabiashara hao watakaoshiriki katika mgomo huo kuwa ni wafanyabiashara wa vyakula, matunda, machinjio ya kuku na bucha za nyama za aina zote sokoni hapo.

error: Content is protected !!