August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wapemba waachwe waone waonavyo

Spread the love

UTHIBITISHO. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amethibitisha. Nini? Kushindwa kutimiza ahadi yake kwa Wazanzibari.

Kama alivyoonesha kuelewa wakati ule alipolihutubia Bunge mjini Dodoma katika kulizindua rasmi, kwamba Zanzibar hakukuwa na utulivu, ndivyo ilivyobakia leo hii kwamba ule mgogoro wa kisiasa unaoiandama Zanzibar ungali mbichi.

Kwa namna alivyozungumza kupitia hutuba yake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Gombani ya Kale, nje kidogo ya mji wa Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, Ijumaa ya 2 Septemba, kilichopo Zanzibar kiuongozi, ndio halali.

Anasema hakuna uchaguzi utakaorudiwa. Ukiuliza Wazanzibari wengi kama walitarajia kusikia kuwepo kwa uchaguzi mwingine ili kurekebisha kinachoaminika kama “usanii” uliofanyika, ni watu mikono miwili-mitatu tu watakaounga mkono.

Hata kwa wanachama kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawaamini kuwa Zanzibar inahitaji uchaguzi mwingine kwa sasa kuliko ile miwili iliyokwishafanywa, ukiwemo ule uliopewa jina kama “uchaguzi wa marudio” ambao ndio umempenyeza Dk. Ali Mohamed Shein kwenye uongozi.

Nimejadiliana na wana-CCM wengi, wa rika na wasifu mbalimbali, kuhusu hali iliyopo Zanzibar baada ya uchaguzi huo wa 15 Machi 2016, na hata sasa, wanasema uchaguzi mwingine hautakuwa ufumbuzi mzuri Zanzibar.

Sasa wao wana-CCM wanaposema uchaguzi mwingine hautaleta ufumbuzi wa hali iliyopo, ina maana moja tu: Zanzibar kuna mgogoro. Nchi hii ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, haijatulia.

Na kama wananchi wenyewe wanaamini nchi yao haijatulia, wakiwa na maana hasa ya kuwa wanaiona misuguano katika jamii, kutokana na yaliyotokea kuhusu uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, ni kwanini basi walazimishwe kuamini kuwa Zanzibar hakuna tatizo lolote isipokuwa wachochezi wa amani?

Kwanza hili neno “amani” naona halijaeleweka sawasawa kwa baadhi ya watu. Wapo wanaodhani amani inajengwa na kuimarishwa kwa maneno zaidi; wanakosea sana. Hivyo sivyo hali halisi ilivyo.

Amani hujengwa kwa maneno na vitendo vinavyoendana nayo hayo maneno. Yakiwa mazuri yanayowapa wananchi matumaini na muongozo kuhusu maisha ya kupendana na kusaidiana huku wakihudumiwa ipasavyo na viongozi wao, maneno yanajenga imani ambayo huzaa amani.

Kwa kujengwa imani, ambayo itatokana tu na wananchi kuwasikia viongozi wao wakipendana na kushirikiana; wakiheshimiana kiutu, na kisiasa wakipingana bila ya kupigana, huku wakitamka yaliyojaa hekima na busara, wananchi watatii viongozi na mamlaka pasina vitisho au nguvu.

Bali hapa upo mtihani mwingine. Mamlaka inayofaa kutiiwa, kwa mujibu wa imani za kiroho, ni ile ambayo wananchi wameiridhia. Nitaeleza vizuri eneo hili.

Kwamba kwa kuwa pana mfumo uliokubaliwa kuwa ndio njia pekee ya kupatikana viongozi wa hiyo mamlaka, wala si viongozi waitwao ‘machaguo ya Mwenyezi Mungu,’ mamlaka inayostahili kutiiwa itakuwa ile ambayo viongozi wake wamepatikana kupitia njia hiyo kwa ukamilifu wa taratibu zinazoelekezwa na mfumo wenyewe.

Mamlaka iliyopatikana kwa utaratibu mwingine usiokuwa wa makubaliano yale, mhh, kwanza inakuwa imejipuuza, na kubwa zaidi, ni kule kujinyima imani ya kuchukuliwa kuwa ndio yenye haki hasa ya kutiiwa na wananchi wanaotoa mamlaka.

Tena, mamlaka yenye ridhaa ninayoikazia jicho kihoja, viongozi wake hawawezi kupata shida zinazoonekana leo Zanzibar, ikiwemo hii ya kiongozi mkuu wa jamhuri kulazimika kutunisha misuli jukwaani akitaka wananchi wampende Dk. Shein.

Huu mwenendo wa kiongozi mkuu kutaka msaidizi wake apendwe tu maana hakuna mbadala, inatoa tafsiri ya waziwazi kuwa ndani ya mamlaka yake, kuna mgogoro. Laiti wananchi wangepewa nafasi ya kusema kwa sauti mbele ya kiongozi mkuu, sina shaka wangesema.

Wananchi ninaowajua wa kisiwa cha Pemba wangesema. Ni watu watulivu, wasikivu, wapole na maridhia, wanasema kile wanachokiamini. Wazanzibari hawa nawajua vizuri hawaogopi chochote kusema ukweli wanaojua. Ndio mila yao!

Ila wa kumwambia huo ukweli, yapasa naye awe msikivu na aongeze sifa nyingine – mstaarabu, muadilifu (mpenda haki) na mvumilivu.

Hawahawa hubaki na upole wao wakiwa mbele ya mtu mkorofi, mjanja, asiyeaminika na anayekosa sifa zile njema. Wapemba wanapobaki wapole, utakosea sana kudhani ni dhaifu. Wanakuwa hivyo kwa sababu kwa asili, wao ni wavumilia maudhi, dhiki na ufisadi.

Hichohicho ambacho kiongozi mkuu amekibaini, kwa kutumia akili ya kuzaliwa au kwa kuambiwa, ndicho kinachompeleka kushangaa “watu hawajui watu wazuri.” Eti hawajui kuchagua kati ya mtu mzuri na mtu mbaya.

Hili wala si fumbo kwao. Wao ni wafumbuzi wazuri wa mafumbo na tungo. Wako mbele kwelikweli kwa kufikiri na kuagua. Si watu wa kutolewa vitendawili vikawa vigumu kwao kutegua. Si wao.

Kwa anayeijua historia yao, hata hatathubutu kuwajibu. Hawajaribiwi. Najua vilevile Wapemba hawatishiwi nyau. Ni watu makini nimesema, wenye upeo mkubwa wa mambo – werevu. Shida ni kwa yule asiyewajua, atajisumbua tu.

Dk. Shein anawajua. Ndio maana ameamua kutulia zaidi kuliko kufanya vinginevyo. Nataka kuamini hata huo utashi wa kusema awatunishie misuli hajaupata. Anajua atakapofanya hivyo, watatulia tu na kuangalia.

Lakini, haitakuwa kwamba wamesalimu amri. Hata kidogo. Wasichokiridhi hawajaribu hata chembe kukipa nafasi. Asilani abadani. Hii ndiyo historia ya kweli kabisa ya watu wa asili ya Pemba. Wanamsimamo. Hawayumbi hata anapotokea mtunisha misuli na kufikiria kuwayumbisha. Kwa hakika si wao wa kuyumba.

Wanajua kuchagua kizuri. Wanajua. Wanajua wanachokitaka, wanajua. Wanajua walipo, walipotoka na watakako kwenda, wanajua. Wanajua lililo jema kwao na baya wanalijua. Wanayajua mabaya watendewayo, wanayajua. Na watawala hata wa tangu enzi, wanawajua Wapemba.

Wao na Wazanzibari wenzao wa Unguja, wale wazalendo wa kweli na wapenda haki, wanajua kwamba Dk. Magufuli sasa ameamua kuwaeleza yaliyo moyoni mwake au anayolazimika kuyasema hata kama hayaamini.

Wanajua si sahihi kusema kwamba uchaguzi umekwisha halafu ikawa kwamba aliyoyasema – Dk. Shein ndiye rais, tena mtu mzuri tu na apendwe huyo – lazima wayaamini. Wameyasikia kwa sababu wamemsikia anayesema hayo, lakini nao si wanaona kwa macho yao?

Wanajua yaliyotokea Oktoba 2015, walichangia. Kadhalika, wanajua kilichotokea Machi 2016, waliona. Wanajua pia waliyotendewa mitaani na majumbani mwao, yote wanayajua.

Anayeona kwa macho yake halazimiki kuambiwa mara mia ‘lile ni dafu.’ Si analiona? Basi aachwe tu aone vile aonavyo. Kwa kuwa wanaambiwa aliyepo ndio yupo mpaka ishiriniishirini, waachwe tu, wala wasidhihakiwe maana nao ni binaadamu.

 

error: Content is protected !!