September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wapangaji waitia hasara CDA  

Spread the love
KWA  kipindi cha miaka minane Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imepata hasara ya Sh. 345 milioni kutokana na wapangaji wa nyumba zinazomilikiwa na mamlaka hiyo kushindwa kulipa kodi, anandika Dany Tibason.
Mbali na wapangaji hao kushindwa kulipa kodi, wameharibu nyumba hizo sambamba na mifumo ya maji na umeme katika nyumba hizo.
Hayo yamebainishwa leo na Angella Msimbila ,Ofisa Uhusiano wa CDA alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mipango ya uboreshaji wa nyumba hizo zipatazo 174 zilizopo maeneo ya Iringa Road.
Amesema kwa kipindi cha miaka 8 wapangaji wa nyumba hizo walikuwa hawalipi kodi kama inavyotakiwa licha ya kuwa kodi waliyotakiwa kulipa ilikuwa kidodo.
Amesema awali wapangaji hao walikuwa wanatakiwa kulipa kodi ya pango sh.22,000 kila mwezi jambo ambalo lilishindikana na hata walipopandishiwa hadi sh.50,000 walipinga.
Angella amesema licha ya kuwa wapangaji hao wamekuwa hawataki kulipa kodi, Mamlaka iliwataka wapangaji hao waondoke katika nyumba hizo ili ufanyike ukarabati lakini walipinga na kukimbilia Mahakamani.
Akitoa ufafanuzi Angella amesema CDA imeweza kushinda kesi na kuwataka wapangaji hao waondoke katika nyumba hizo kwa kupewa muda wa miezi 3 ili kuwezesha ukarabati ufanyike.
Amesema pamoja na amri halali ya mahakama CDA iliwaongezea tena siku saba wapangaji hao kuondoka   ,siku hizo zimeshaisha jana.
“Kwa sasa CDA imetangaza tenda ya kufanya ukarabati katika nyumba zetu ambazo zimechakaa sana na hazifai kuendelea kutumika, tunataka kufanya ukarabati mkubwa zaidi.
“Zile nyumba siyo kupiga rangi tu, bali kuna kazi kubwa ya kubadilisha mifumo ya umeme, kutengeneza miundombinu ya maji na mambo mengine, kwa maana hiyo haiwezekani kufanyika kwa ukarabati mkubwa hivyo watu wakiwa ndani’’ amesema Angella.
Amesema kuwa baada ya kufanyika kwa ukarabati huo nyumba hizo zitapangishwa kwa viwango ambavyo vinatakiwa kwa sasa hata hivyo watakao pewa kipaumbele ni wale wapangaji wa mwanzo kama wataona wanakubaliana na masharti ya upangaji wa nyumba hizo.
Kwa upande wa mpangaji ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema licha ya kuwa wanalipa kodi ndogo lakini nyumba hizo zimechoka.
Amesema kitendo cha CDA kutaka kurekebisha nyumba hizo kitasaidia watu kuishi katika nyumba ambazo ni bora na imara.
“Hizi nyumba kwa sasa hazifai yaani hata TV unaogopa kuwasha kutokana na mifimo ya Umeme kuwa mipovu, si mifumo tu kuwa mibovu hata vyooni hapafai hata kidogo hivyo ni bora kuhakikisha ukarabati unafanyika na kama tutahitaji kupanga tena tutaomba maadamu wamesema watatupa kipaumbele sisi sawa hakuna neno” amesema mmoja wa wapangaji wa nyumba hizo.
error: Content is protected !!