July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wapambe wakuu wa Lowassa kitanzini

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa

Spread the love

MAKADA wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walio pia vinara wakubwa wa kumuunga mkono waziri mkuu aliyejiuzulu kwa shinikizo la bunge mwaka 2008, Edward Lowassa, katika kampeni ya kusaka urais wa Tanzania, wamehojiwa kwa saa kadhaa na Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho mjini Dodoma. Anaandika Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kamati hiyo tangu jana ilikuwa katika vikao vyake ikichambua majina ya makada wa CCM walioomba uteuzi wa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Upepo ulibadilika kuanzia asubuhi leo baada ya wapambe wa Lowassa kukutwa wanaitwa kuripoti mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.

Kamati hiyo pia inamjumuisha Katibu Mkuu Kanali Abdulrahman Kinana, mwanasiasa ambaye amekuwa wazi katika kupinga mwenendo wa ukiukaji wa taratibu za kuendesha mambo ndani ya chama ikiwemo suala la harakati za kutafuta uteuzi wa kugombea urais.

Mmoja wa makada-wapambe wa Lowassa waliohojiwa na kamati hiyo kuhusu masuala ambayo hayakuwekwa wazi na uongozi wa CCM, ni Kingunge Ngombale-Mwiru, kiongozi mstaafu aliyepata kuwa waziri wa serikalini na mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Taarifa kutoka mjini Dodoma zimesema kwamba Kingunge ambaye amebadilika safari hii na kuwa muungaji mkono maarufu na wa waziwazi wa Lowassa, alihojiwa kwa saa mbili, akianzia saa 8 mchana.

Kingunge alijitokeza hadharani akimtetea Lowassa dhidi ya tuhuma za ufisadi na matumizi ya fedha katika harakati za kutafuta urais na juzi alisema wazi kuwa angependa kuona chama kinatenda haki kwa wagombea wakati huu kinapofanya vikao vya maamuzi mjini Dodoma.

Maelezo yake yamejenga taswira kwamba huenda Lowassa akaenguliwa mapema kabla ya kufika kwenye NEC, matokeo anayoamini yatakuwa ni kumuonea kwani “hana ubaya wowote na kama ni fedha basi na wenzake pia wanatumia fedha.”

Makada wengine waliohojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja ambaye aliingia kikaoni baada ya Kingunge kutoka kuhojiwa.

Hao wamekuwa wakisikika mara kwa mara wakishambulia wenzao walio katika makundi mengine ya wasaka urais ndani ya chama hicho, kiasi cha baadhi yao kumfungulia kesi Paul Makonda, kijana wa CCM ambaye amejipatia umaarufu kwa kumshambulia Lowassa, akisema ni kiongozi asiyefaa kutokana na kupenda kutumia pesa kutafuta uongozi.

Lowassa ni mmoja wa makada sita waliofikishwa mbele ya Kamati ya Usalama na Maadili ya Mangula kwa tuhuma za kukiuka taratibu za kutafuta urais na wakapewa adhabu ya kutogombea uongozi kwa miezi 12, lakini adhabu hiyo ilikwenda mpaka hivi karibuni ilipotangazwa kuwa imeondolewa.

Lowassa ambaye alilazimishwa kujiuzulu kufuatia kashfa ya kuingilia utaratibu wa zabuni ya mkataba wa kufua umeme iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond, iliyothibitika kutokuwa na uwezo wa kifedha, vifaa na utaalamu, amekuwa akilaumiwa na wakuu wa chama kwa kutumia fedha kugawa chama akikusanya makundi ya wanachama.

Mbali na Lowassa, wengine waliowekwa kitimoto na Chama ni Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri wa Kilimo, Steven Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Wote hao wameomba kuteuliwa kugombea urais.

error: Content is protected !!