July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waonywa matumizi ya mifuko ya plastiki

Mifuko wa plastiki ikitupwa tayari kwa kuyateketeza

Spread the love

WANANCHI wameshauriwa kutotumia mifuko ya plastiki na vifungio vyake kwa ajili ya kuwekea au kuifadhi chakula na badala yake watumie vifungashio vya glasi na chuma isiyoshika kutu na vyombo vingine vya asili.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Maselle, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa Kimwanga (CUF).

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inasema nini kuhusu tatizo kubwa la uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki.

Pia, alitaka kujua kama kuna madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula cha moto kwenye mifuko hiyo.

Akijibu swali hilo, Maselle amesema madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula cha moto katika mifuko ya plastiki ni pamoja na kuwepo kwa uwezekano wa kemikali zilizotumika kutengeneza mifuko hiyo kuingia kwenye chakula na kukifanya kuwa na sumu.

“Sumu hii yaweza kusababisha saratani, kuharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi hususani kwa watoto ambao bado kuzaliwa, mabadiliko ya kijenetiki, matatizo ya kushindwa kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa wa tabu au kutokamilika na ini kushindwa kufanyakazi vizuri,” alisema.

Ametaja magonjwa mengine yanayoweza kusababishwa na mifuko hiyo kuwa ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa utendaji wa figo na magonjwa yanayaohusiana na mfumo wa kupumulia.

Kuhusu uchafuzi wa mazingira, amesema serikali inatambua kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.

Maselle amefafanua kuwa, ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo yenye unene wa chini ya maikroni 30 na kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala.

error: Content is protected !!