May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waomba vikwazo dhidi ya watu wenye ulemavu viondolewe

Spread the love

 

TAASISI ya Vijana Wenye Ulemavu (YoWDO), imeIomba Serikali na jamii kwa ujumla, iondoe vikwazo vinavyosababisha kundi hilo lisishiriki kwenye shughuli za maendeleo ya Taifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 1 Machi 2022, jijini Dar es Salaam, katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu watu wenye ulemavu, iliyoandaliwa na YoWDO.

Mkuu wa Programu wa YoWDO, Genarius Ernest, amesema watu wengi wenye ulemavu wanaachwa katika fursa za kimaendeleo, kutokana na kuwekewa vikwazo ndani ya jamii kutokana na hali yao.

“Kumekuwa na mtizamao katika jamii kwamba watu wenye ulemavu hawawezi, hivyo wanakumbana na vikwazo vilivyotengenezwa na jamii. Ili tumsaidie asikumbane na vikwazo  tubadilike, tuondoe vikwazo ili tuweke mazingira jumuishi,” amesema Ernest na kuongeza:

“Shida kubwa ni hii hapa, ukiwa na jamii yenye mtazamo hasi, hii jamii itatengeneza sera mbovu, hizi sera ndiyo zinatengeneza mitazamo hasi. Tukiondoa mitazamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu, tutatengeneza jamii nzuri,” amesema Ernest.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa YoWDO, Rajab Mpilipili, amesema kundi hilo linakabiliwa na changamoto ya kuachwa katika fursa za maendeleo, hasa za kielimu na kiuchumi.

Kwa kuwa jamii imeweka dhana potofu dhidi yao, kuwa hawawezi kufanya shughuli za kimaendeleo kutokana na ulemavu wao, kitu ambacho si kweli.

“Kumekuwa kunatolewa lugha mbaya juu ya watu wenye ulemavu, kitendo kinachopelekea wajione wanatengwa. Lugha nzuri itawafanya wenye ulemavu kujihisi wanathaminiwa na kuchukuliwa kama watu. Hii  Itasaidia kujenga jamii jumuishi,” amesema Mpilipili.

Mpilipili amesema watu wenye ulemavu wana haki ya kupata fursa za maendeleo sawa na watu wasiokuwa na ulemavu, ikiwemo ya kuajiriwa, kufanya biashara, kupata elimu na afya.

Wakati huo, Mpilipili amewaomba wananchi waache kuwaita watu wenye ulemavu majina yanayotweza utu wao.

“Tunaendelea kushirikiana kuijenga jamii yenye usawa, inayoheshimu kila mtu na ushiriki sawa katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. YoWDO imeanzishwa kuhakikisha vijana wanapata haki sawa sawa na watu wengine,” amesema Mpilipili.

error: Content is protected !!