December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanusurika kifo kwa kuchomwa moto kisa wivu wa mapenzi

Spread the love

 

WINIFRIDA Wambura, na watoto wawili, wamenusurika kufariki dunia baada ya mkwe wake, Naim Byabato, kuchoma moto nyumba kwa sababu ya wivu wa mapenzi.Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tukio hilo limetokea usiku wa Jumamosi, tarehe 29 Oktoba 2022, katika Kata ya Muhongolo, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, baada ya Babyato kupishana kauli na aliyekuwa mwenza wake Teckla Athanas, ambaye ni binti wa Winifrida.

Akizungumza kwa njia ya simu na MwanaHALISI Online, Leo Jumapili, tarehe 30 Oktoba 2022, Winifrida amedai mkwe wake huyo alitekeleza tukio hilo majira ya saa 2.00 usiku, ambapo alimwaga mafuta ya petroli Kisha kuanza kuchoma moto.

Winifrida amedai, walinusurika kifo baada ya majirani kuja kuwasaidia kuzima moto uliokuwa umewaka, wakati yeye na mtoto wake pamoja na mjukumuu wake ambaye ni mtoto wa Byabato, wakiwa ndani.

“Majira ya saa mbili usiku mtoto wangu wa darasa la nne akaniambia mama nasikia harufu ya mafuta ya petroli Kisha na mimi nikaisikia, wakati huo tulikuwa ndani milango tumeifunga na Binti yangu Teckla alikwenda harusini. Baada ya kusikia harufu wakati nataka kutoka nje nikakuta moto mlangoni unawaka Kisha nikasikia mtu anakimbia kuangalia dirishani nikamuona Byabato anawasha dirisha nikamwambia baba Farida unataka kutuuwa, hakujali akaendelea kuwasha. Nikapiga kelele kuomba msaada kwa majirani, waliwahi kuja wakasaidia kuzima moto Kwa mchanga,” amedai Wikifrida.

Amedai, kabla Byabato kutekeleza tukio Hilo, alimpigia simu Teckla akimtaka wakutane Kahama Mjini, ili amuone mtoto wake pamoja na kumpa pesa ya matumizi, lakini Binti yake alikataa kuonana naye na kumwambia aende nyumbani kwao.

Winifrida amedai, baada ya binti yake kukataa kukutana na mwenza wake huyo wa zamani, Byabato alimtolea vitisho akimwambia asipoenda atachoma nyumba Yao au kuwachinja wazazi wake.

“Yule mwanaume ni mkwilima wangu, ameishi naye miaka Saba na amezaa naye watoto wawili. Walianza kuishi kuanzia 2014 hadi 2021, baada ya Binti yangu kurudi nyumbani kutokana na manyanyaso kuzidi,”

” Mida ya saa 11.00 jioni Byabato alimwambia Binti yangu kwamba Yuko Kahama mjini aende kuchukua pesa ya matumizi ya mtoto na kwamba anataka kumuona mototo wake, mwanangu akamwambia Mimi siwezi kuja nenda nyumbani utamkuta mtoto wako,” amedai Winifrida.

Amedai “baada ya Binti yangu kukataa, akamwambia nitakukomesha, nitamchinja baba Yako na mama Yako. Nitakupa hasara nitachoma nyumba, lakini tulipuuza vitisho hivyo kwani alikuwa amelewa.”

Winifrida amedai, baada ya tukio Hilo alimpigia Binti yake arudi nyumbani, alirudi na kuambatana naye Hadi Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Kahama, kwa ajili ya kuripoti.

Amedai, wakati wako Polisi Byabato alimpigia tena simu Teckla akimtaka wakutane, ndipo Binti yake alikubali na kwenda na Polisi hadi eneo la tukio kisha mtuhumiwa huyo kufanikiwa kukamatwa.

Kwa upande wake Teckla, amedai Byabato alikuwa na desturi ya kumfanyia vitendo vya ukatili tangu akiishi naye na hata baada ya kurudi nyumbani kwao.

“Sio mara ya kwanza kunitishia, mara nyingi amekuwa ananitishia kuniuwa, wakati mwinginr tukigombana ananishikia kisu akiniambia hata ukinipeleka Polisi nitatoka kwetu watanitoa. Hata kwake niliondoka sababu ya vitisho na manyanyaso,” amedai Teckla.

MwanaHALISI Online imejitahidi kulitafuta Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kwa ajili ya taarifa zaidi kuhusu tukio hilo, lakini halikufanikiwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbulu, Hamza Abdallah, amesema amepata taarifa za tukio hilo kutoka Kwa majirani na kwamba alipowatafuta wahusika Kwa njia ya simu kuwauliza kuhusu jambo Hilo, simu zao hazikupatikana.

Baadhi ya majirani katika mtaa huo, wamethibitisha kutokea Kwa tukio Hilo na kudai kama juhudi za kuwaokoa wahusika zisingefanyika Kwa wakati huenda Winifrida na watoto hao wawili wangepotesha maisha.

error: Content is protected !!