June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanne tuhumani kusafirisha nyara

Spread the love

SERIKALI imefikisha mahakamani watu wanne ikiwatuhumu kwa kosa la kusafirisha nyara za serikali kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Julai 5 mwaka huu. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Watu hao walisomewa mashitaka leo na Wakili wa Serikali, Salim Msemo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akiwataja watuhumiwa kuwa ni Clemence Jingu Mbaruck (46), Emmanuel Nyambale Nsanganiye (54), Salum Seif Mnyones (33) na Albadri Habibu Mshana ambao wote ni walinzi kwenye uwanja huo.

Wakili Msemo akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Huruma Shahid, alidai kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kusafirisha meno ya tembo kilogramu 150 yenye thamani ya Dola 85,110.21, meno ya simba yenye thamani ya Dola 27,079 na kucha 35 za simba zenye thamani ya Dola 15,145.

Thamani ya jumla ya mali zote imetajwa na wakili wa serikali kuwa ni Dola 127,334 kiasi ambachoni sawa na Sh. 267,401,400 za Tanzania.

Shitaka jingine ni kosa la kusafirisha nyara bila ya kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Watuhumiwa hao hawakutakiwa kusema chochote kwa kuwa mashitaka yao yapo mahakama hiyo kwa hatua ya uchunguzi. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 29 mwaka huu itakapotajwa, na watuhumiwa kurudishwa rumande.

Serikali inawakilishwa katika kesi hiyo na jopo la wanasheria wake wakiwemo pia Wankyo Simon na Faraji Nchimbi.

error: Content is protected !!