July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wangekuwa darasani wasingekuwa barabarani

Wanafunzi wa darasa la pili wakiwa darasani

Spread the love

MIAKA miwili iliyopita nikiwa sekondari, nilikuwa nikipata wakati kujadiliana na wanafunzi wenzangu kuhusu maisha ya nyumbani mbali na yale ya kuonana na kukaa darasani asubuhi hadi mchana.

Mara nyingi ilikuwa katika muada ambao hatukuwa na mwalimu darasani au hakukuwa na kipindi. Tulikuwa tunaibua hoja na kujadiliana kama hatua ya kuchangamsha akili zetu.

Nayakumbuka vema maneno ya mmoja wa rafiki zangu (wa kiume). Aliniambia kama si vile kuja shule kila siku, basi wakati ule tunapiga soga au mwalimu yupo darasani anasomesha, yeye angekuwa na jembe shambani. Kwamba yuko katikati ya tope au dongo gumu analima.

Alikuwa na maana kuwa ugumu wa maisha kwake na familia yao usingemruhusu kukaa nyumbani bila ya kupewa jembe. Angebeba jembe ili kuungana na wazazi wake katika kilimo chao cha kujikimu.

Februari mwaka huu, vijana wasio kazi katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam wakijiunda katika kundi lililoitwa Panya Road, walisababisha taharuki kubwa maeneo ya Sinza, Kigogo, Tabata, Magomeni na Kinondon. Wengine waliishia vituo vya polisi na baadaye ifanyika operesheni kabambe ya kuwatia nguvuni ilipobainika ni mtandao.

Juzi waliibuka vijana eneo la Tabata wakazusha tafrani kama ile. Walipora wananchi mali zao na kujeruhi baadhi yao.

Wakati ule niliposoma habari kuhusu kijana Mohamed Ayubu (19) ambaye mwili wake ulikutwa na majeraha ya kupigwa maeneo ya Tandale akiwa ameshaaga dunia, na habari ile ikasema Ayubu aliacha shule akajiingiza katika vikundi vya wahuni, haraka nikamkumbuka yule rafiki yangu shuleni.

Kumbe hata kama Ayubu angekuwa shule, asingepata nafasi ya kujumuika na Panya Road.

Rafiki yangu alinambia kama si shule, angekuwa anatoka na jembe kila siku asubuhi kwenda shambani. Aliamini kwamba kuwa kwake shambani, ni adhabu hasa kwa kuzingatia kuwa jembe analotumia si la trekta bali la mkono, hivyo shule ilikuwa inamuepusha na kazi ile aliyoiyona ngumu.

Umasikini si sababu inayokubalika kuwa wewe ndio uwe na haki ya kupora na kuiba. Wakati mwengine usilazimishe wizi kuwa ndio kazi ya kipato kila siku kwani unahatarisha kuishia kuchomwa moto au kurogwa.

Unaweza kuumwa maradhi yasiyo tiba. Unahangaika kila hospitali huponi, kumbe unatumikia laana ya Mwenyezi Mungu, kutokana na dua za watu wema uliowavamia na kuwaibia, pengine huku wakiwajeruhi.

Kama kijana anafika Dar es Salaam kutafuta maisha na akakaa miaka mingi bila ya kupata kipato cha maana, bora arudi kijijini akaanzishe kilimo. Nguvu zake za kubeba mapanga au mapande nondo ni bora na kheri kama utaenda kubeba jembe.

Sisemi haya kwa dharau na kejeli lakini kwa akili yangu nahisi kwenda kijijini ukaanzisha kilimo au mifugo ni bora zaidi kuliko kukaa Dar kuvuta bangi, kupora na kuharibu mali za watu. Utakufa!

Kijana rudi kijijini, maisha si mjini tu. Kilimo cha mchicha au nyanya kinasaidia kupata kipato cha uhakika. Ukimuona bilionea Bakhresa na wengine basi usidhani kuwa wamekuwa vile kwa sababu ya kukaba, wameanza chini sana hata ukielezwa walikoanza huwezi kuamini.

Hawa Panya Road ni vijana wadogo ambao wakati ule wanatembea barabarani na mapanga, nondo, bisibisi, sime, marungu kwa kweli ilipasa wale waliomaliza shule wawe wanaingia viwandani kunakofanyika uzalishaji wa nguo, vipuri na kuunganisha saa za mkononi na ukutani.

Wale wenye umri wa kupasa kuwa shuleni kwa masomo, na kutafuta madaftari mapya ili kurudi shule kwa mwaka mpya wa masomo 2015, au wawe katika muhula wa kwanza mwaka wa tatu chuoni wakisubiri mitihani ya mwisho wa simesta.

Inaweza kuwa hali ya maisha imemsukuma kijana aache shule, lakini haijawa sababu ya kuwa na haki ya kuiba. Nirudie kusema maisha sio Dar tu. Mtu anaweza kuhamia Korogwe, Bariadi, Kanyarwe (Bukoba), Misungwi (Mwanza), Vigwaza na Mzenga (Pwani) na akafanya shughuli ya maana kiuchumi kuliko kuiba, kupora na kujeruhi wananchi Mbagala, Kurasini, Tandika, Buguruni, Manzese na Kinondoni.

Vijijini ardhi zina mbolea za kutosha, huenda pembejeo za serikali zikakufikia, miradi ya “kilimo kwanza” na ufugaji wanyama na nyuki huenda yakawa ndio mambo yatakayokutoa ulipo, si lazima ung’ang’anie Dar.

Kama umasikini ndio unampa akili za kuiba, hayo si maisha na wala hizo si akili. Usitarajie serikali ya Bongo siku moja itafika kukushika mkono kijiweni Mbagala au Ilala cha kuvuta bangi na kukwapua ikakupe ajira.

Serikali yenyewe inadaiwa. Kila mwaka inasamehewa madeni, watu wanatia umasikini nchi. Usitegemee serikali ikukomboe kama hujafanya juhudi binafsi. Jitahidi utapata cha halali. Mishemishe na uporaji itakupeleka kaburini.

Kwa upande mwengine, kila mtu ana jukumu kuhakikisha matatizo yanaondoka. Nadhani matatizo yenyewe yanasababishwa na kuchanganyikiwa (kisaikolojia) shauri ya maisha magumu mtu anayopitia, au madawa avutayo.

Yawapasa wazazi watambue wapi watoto wao wanalala, nini wanakula, isijekuwa baada ya ugali na matembele ya mchana, pia naye anaenda kula unga ambao si ugali.

Kisa cha Ayubu kinaonesha wazi upungufu wa wazazi katika kulea vijana wao. Baba au mama ajue nyendo za  mtoto wake,  anakuwa wapi kutwa, wacheza wenzake ni nani. Aliacha shule lakini hazikuonekana juhudi za wazazi kumrudisha.

Watoto wengine huacha shule bila ya sababu za msingi, huamua tu kuacha na mzazi haoneshi kiu ya kumrudisha. Kaacha na yeye anamuacha kama alivyo acha, jamani huo si ulezi ni ufugaji.

Mtoto anapaswa kulelewa si kufugwa. Malezi yawe tofauti na kufuga ng’ombe kama wale wa Wamaasai. Ng’ombe hupewa kula na kutafutiwa pa kulala. Mtoto yeye hupewa kula na kufuatiliwa nyendo zake kabla na baada ya kula. Njia hiyo itakusaidia mzazi kumuepusha mwanao na Panya Road.

Lakini mtoto kumuacha tu afanye atakalo, aingie ndani muda atakao hata saa saba usiku, usijue kutwa anashinda wapi, na nani na wanafanya nini. Wewe unampa kula na kitanda. Utazalisha Panya Road na Mbwa mwitu nyumbani.

Inasikitisha vijana wadogo ndio wanashika mapanga mitaani wakikata kata watu kama tungule.

Serikali nayo inapaswa kuonesha juhudi za ziada kutatua tatizo la malezi, badala ya kudhani kukamata na kushitaki vijana, ndio dawa ya kudhibiti vijana waovu.

Hatua hiyo itatuliza mwaka, wakizaliwa na kukua mwaka mwengine watoto kama hawa, wanaingia tena mitaani. Viongozi wanajua zaidi sababu za watoto kuwa mitaani na njia za kuwasaidia.

Elimu ni jambo la msingi. Wazazi wahakikishe watoto hawaachi shule. Japo wapo wenye elimu ndio hao wanaoiba mabilioni ya pesa lakini wapewe elimu wakiiba mabilioni tutajua vya kupambana nao huko juu.

Makala hii imeandikwa na Rashid Abdallah ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM)

error: Content is protected !!