July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanawake tushiriki kampeni – Mongela

Spread the love

MTANDAO wa Wanawake, Katiba na Uchaguzi (T-WCP/Ulingo), umehimiza wanawake nchini kushiriki kikamilifu mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera za wagombea zinazohusu masuala ya wanawake na kuzichambua. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Hayo yalielezwa katika tamko lao leo jijini Dar es Salaam kuhusu kampeni za uchaguzi mkuu zinazoanza kesho kwa ajili ya kumchagua rais, wabunge na madiwani. Kwa Zanzibar, pia watapiga kura kuchagua Rais wa Zanzibar na wawakilishi.

Katibu Mkuu wa Mkutano wa Wanawake Duniani wa mwaka 1995 Beijing, Getrude Mongela, akisoma tamko hilo, alisema ni vyema serikali ikashirikisha wanawake katika mambo ya uongozi bila ya kujali jinsia kwani wanao uwezo wa kuongoza, sawa na wanaume.

Mongela ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika nchini Afrika Kusini, alisema Ibara ya 66(1)b ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inataka idadi ya wabunge wanawake isipungue asilimia 30, wanawake walioteuliwa kuwania ngazi tofauti za uongozi na wanaostahili wanatakiwa kupewa nafasi ya ushindi.

Amevipongeza vyama vilivyoamua kutoa nafasi kwa wagombea wanawake katika ngazi zote na kuwahimiza wanawake walioteuliwa waoneshe uwezo wao kwa kuchapakazi kwa bidii ili kuthibitishia jamii kwamba ni viongozi makini na waadilifu.

“Hatutachagua kiongozi tu kwa kuwa ni mwanamke, tutachagua kiongozi mwenye uwezo wa kutekeleza ajenda yetu,” amesema Mongela akimaanisha kuwa mgombea bora kwao ni yule anayejitokeza waziwazi kutambua na kutetea mambo yenye maslahi kwa wanawake nchini kote.

Mongela amesema wanawake wakishiriki kikamilifu kampeni watapata fursa ya kuchanganua sera za viongozi wao ili kujipa nafasi ya mbele kama wanawake katika kutoa dukuduku kuhusu matatizo yanayokwamisha maendeleo ya wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi amesema vyama vya siasa vinatakiwa kuendesha kampeni kistaarabu, zinazoheshimu misingi, sheria na siasa za ushindani zinazotambua kushinda na kushindwa na kwa yule atakayeshindwa, ayakubali matokeo.

Liundi amesema wagombea waache kutumia nguvu ya fedha kununua kura bali watumie nguvu ya hoja kuwashawishi wapigakura wawachague, pamoja na kueleza jinsi watakavyotekeleza changamoto zinazowakumba wananchi.

“Serikali iweke taratibu za kuwezesha wananchi wenye mahitaji maalum, wakiwemo wasioona, viziwi, wenye ulemavu wa ngozi, wajawazito, watoto na wazee wanaoshiriki katika uchaguzi kama wapiga kura,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la utetezi la wanawake, Avemaria Semakafu amesema sera zinazomjali na kumtazama mwanamke na jamii nyingine za watu dhalili, ndizo zizingatiwe katika kuchagua.

Semakafu amesema suala la ubunge na udiwani ni uwakilishi wa umma na sio chama, hivyo ni muhimu wagombea watoe ahadi ya kweli ya kumwangalia mwanamke apate nafasi ya kugombea ubunge katika jimbo badala ya kusubiri apewe vitia maalum.

Ametaja pia tatizo la vifo vya watoto na akinamama kama kilio kinachohitaji ufumbuzi wa kudumu kwa sababu kinasababisha athari kubwa.

Ajenda za wanawake nchini Tanzania zimekuwa ni pamoja na kuondolewa kwa sheria kandamizi ya ndoa ya mwaka 1971, uzazi salama, usawa kati ya mwanamke na mwanamume katika ajira, umilikaji raslimali ikiwemo ardhi na urithi.

error: Content is protected !!