July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Wanawake bado wananyimwa haki’

Wamawake wakijishughulisha na kilimo cha mbogamboga

Spread the love

IMEELEZWA kuwa jamii nyingi nchini hususani jinsi ya kike, imekuwa ikinyimwa haki zao za msingi ikiwemo umilikaji wa ardhi hali ambayo imekuwa haileti taswira nzuri katika jamii. Anaandika Doreen Aloyce, Arumeru (endelea). 

Hayo yalibainika katika semini ya wakulima na wafugaji wilayani Arumeru, iliyoandaliwa na Shirika la kusaidia jamii kutambua haki zao (CEDESOTA) kwa lengo la kuwaelimisha na kubaini changamoto zilizomo ndani ya jamii ya Wameru.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wamelishukuru shirika hilo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiwapatia elimu ya kutosha juu ya haki zao pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.

Magreth Pallangyo na Yunis Mbise, walisema kuwa wamezitambua haki zao na kuweza kudai pale kunapostahili, kwani mpaka sasa jamii yao haimtambui mwanamke kama mmliki wa kitu, badala yake inamtambua kama wa kuolewa tu.

Waliongeza kwamba, hapo awali mila zao zilikuwa gandamizi huku wakinyanyaswa bila kutambua wakimbilie wapi, hawakujua sheria ya ardhi hata kama wamefiwa na waume zao walinyang’anywa na kufukuzwa, lakini kupitia mafunzo hayo watakwenda kuelimisha wanawake wengine na jamii kwa ujumla kwani tayari wamepata mwanga wa kujua sheria.

Nao wenyeviti wa vijiji pamoja na mabaraza ya ardhi, wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa wamekuwa wakinyanyaswa sana bila kutambua wajibu wao.

“Tumekuwa tukishindwa kutatua kesi za ardhi, zikitoka ndani ya kijiji na kupelekwa kwenye kata nyingine kusikilizwa huku wakiacha kijiji husika, hali ambayo imekuwa ikiwajengea wengi mazingira ya rushwa,” amesema.

Mkurugenzi wa CEDESOTA, Jackson Muro, amesema mafunzo hayo ni kwa lengo la kuwaelimisha wakulima, wafugaji, wenyeviti wa vijiji na mabaraza ya ardhi ili kuweza kujua na kutambua haki zao za kumiliki ardhi, kwani wengi wamekuwa wakidhulumiwa bila kujua haki zao.

Muro ameongeza kuwa, kwa muda mrefu wanawake katika jamii wamekuwa hawapati haki ya umiliki wa ardhi na mara baada ya kufanya utafiti katika kabila la Wameru, akagundua nao tatizo hilo halijaisha ndipo akachukua jukumu la kuwapa semina hiyo ili kuwapa mbinu za kutatua migogoro hiyo.

Ameitaka jamii kuepukana na mila potofu ambazo zinawagandamiza wanawake huku ikitambua kila binadamu ni sawa na wajibu wa kumiliki kitu chochote kama wanaume.

error: Content is protected !!