July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanavyuo ‘wamrudi’ Prof. Ndalichako

Spread the love

LICHA ya Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kusimamisha kazi wakurugenzi wanne wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), wanavyuo nchini wamesema, hatua hiyo haitoshi, anaandika Regina Mkonde.

Wanasema, Prof. Ndalichako kachuku hatua nzuri lakini huwenda isizae matunda kutokana na kuwepo watumishi wengine walio na tabia sawa na wale waliosimamishwa kwenye taasisi hiyo.

Wakizungumza na MwanaHalisi Online kwa wakati tofauti, wameeleza kuwa tatizo la bodi siyo wakurugenzi pekee bali watumishi wa chini wakidai kuwa mzizi wa matatizo yao.

Yohane Fulgence Kihaga, Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Muhimbili, amesema, ili changamoto hizo ziishe, serikali haina budi kuwawajibisha watumishi wa chini.

“Bodi inakabiliwa na changamoto nyingi, kitendo cha Prof. Ndalichako kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne hakitasaidia kuondoa changamoto hizo, inabidi aondoe mizizi ambao ni watumishi wa chini,” amesema Kihaga.

Isaya Mwakatuma, Wziri wa Mikopo Chuo cha Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam amesema, utendaji wa watumishi wa bodi kuanzia watumishi wa chini hadi wakurugenzi hauridhishi.

“Adhabu waliyopewa wakurugenzi ni ndogo, wametutesa sana wakishirikiana na watumishi wa ngazi za chini, wamechangia kuharibu utendaji wa bodi,” amesema Mwakatuma.

Chrisantus Philbert, Waziri wa Mikopo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) amesema, kumekuwepo na uzembe baina ya watumishi wa ngazi za chini na wakurugenzi na kwamba, umechangia kuongeza tatizo la uchelewaji mikopo.

“Uzembe wa wakurugenzi na watumishi wake ulichochea matatizo ya uchelewaji wa mikopo, serikali inabidi ifumue uongozi wa bodi na kuunda uongozi mpya inaweza ikasaidia,” amesema Philbert.

Wanafunzi wa elimu ya juu nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za mikopo ikiwemo changamoto ya bodi kuwapa mikopo wanafunzi waliomaliza.

Joel Ntile, Waziri wa Mikopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema, pamoja na hatua hiyo, taasisi ya mikopo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na wanaostaili kupata mkopo kupewa asilimia chache ama kutopata kabisa.

“Lakini pia hata kwa wale wanufaikaji wa mikopo bado kuna changamoto kubwa ya ucheleweshaji pesa za wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini,” amesema.

Theodory Faustine, Kitivo cha Taarifa na Teknolojia za Mawasiliano UDSM amsema, kufukuzwa kwa viongozi waandamizi wa bodi ya mikopo ni hatua nzuri kwa kuwa nategemea kuona ufanisi katika bodi.

“Nataka kuona matatizo ambayo yalikuwa yakilalamikiwa hapo nyuma kama ucheleweshwaji wa stahiki za wanafunzi wa elimu ya juu yanakomeshwa,” amesema.

Sammy Omar, Mwanachuo wa UDSM amesema, uamuzi uliochukuliwa ni wa busara kwa kuwa mabadiliko hayo yalihitajika siku nyingi.

“Lakini hofu yangu ni kwamba haya yanayofanywa na waziri yasije yakawa ni msukumo tu wa Rais,” amesema na kuongeza “tunachohitaji sio tu wabadilishwe watendaji bali utendaji wenyewe uwe wa kiuadilifu.”

error: Content is protected !!