June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanavyojadili Siku 100 za Rais Magufuli

Spread the love

MKWAMO wa kisiasa visiwani Zanzibar umetia najisi sifa na mafanikio ya Rais John Magufuli katika siku 100 alizokuwepo madarakani zinazofikia kesho tangu aapishwe tarehe 5 Novemba mwaka jana, anaandika Faki Sosi.

Waliotoa maoni yao kwa MwanaHALISI Online wametofautiana mtazamo kuhusu siku 100 za Rais Magufuli madarakani huku wengine wakisema ameshindwa kufikia maratajio ya wengi hususani utatuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Alhad Mussa, Sheikh Mkuu wa MKoa wa Dar es Salaam amesema kuwa siku 100 za Rais Magufuli ni za baraka na neema kwa Watanzania na kwamba zimetoa nuru na heshima kubwa kwenye serikali yake.

Amesema, ameokoa kiasi kikubwa cha fedha na kwamba Watanzania watafurahia keki ya Taifa ambapo ameshauri wananchi kushikamana na kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu.’

“Kauli mbiu hii imeridhiwa na Mungu kwani Mungu aliumba mbingu na ardhi kwa kuashiria kuwa kazi ni wajibu,” amesema Sheikh Alhad.

Dk. Benson Bana ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema, siku 100 za uongozi wa Rais Magufuli amevunja rekodi ya kuwa rais pekee Afrika mwenye utendaji wa kasi lakini pia ametofautiana na watangulizi wake kiutendaji.

“Rais Magufuli amekuwa ni tumaini kwa Watanzania, ndani ya siku 100 amewawajibisha watumishi waandamiza zaidi ya 190,” amesema Dk. Bana.

Hata hivyo, kuhusu mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar Dk. Bana amesema, Rais Magufuli hapaswi kulaumiwa kutokana na kwamba yeye anajua kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndio iliyo na mamlaka na uchaguzi huo.

Amedai kwamba ZEC inaweza kusimamia suala hilo na kwamba anazitaka nchi za Ulaya zisipewe nafasi kuingilia mgogoro huo kwa kuwa zinaweza kuuzidisha.

Profesa Abdul Sharrif ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar (BAKIZA) amesema, katika siku 100 za Rais Magufuli hakufanya cha ajabu.

Amesema siku hizo 100 za Rais Magufuli ni kama amekuja kusalimu na kusimamisha watu kazi huku akikwepa nafasi yake ya kutatua mgogoro wa Zanzibar kwa kudai hana mamlaka wakati vurugu zitakapozuka, atatumia majeshi yake kwenda kuzizima.

“Majeshi ya Jamhuri ya Muungano ndio yaliyoua Wazanzibari mwaka 2001 na hayo hayo yanaweza kutumika tena kufanya kile kilichofanywa mwaka huo,” amesema.

Prof. Sharifu amemsifu Ibrahimu Kaduma ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa mkweli na kujitokeza mbele ya umma.

Amesema kuwa, hatua ya Kaduma kusema kwamba chama chake (CCM) kimeshindwa na kiwaachie walioshinda ni ujasiri ambao alipaswa kuwa nao Rais Magufuli na ingeleta tija kwa taifa.

Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu nchini amesema kuwa, Rais Magufuli ameonesha nia ya kutaka uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Amesema, pamoja na hivyo lakini ameshindwa kusimamia utatuzi wa mgogoro wa kisiasa unaondelea Zanzibar na kwamba, visiwani humo kumetokea uvunjifu wa katiba uliofanywa na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC.

Sheikh Ponda amesema kuwa, kiongozi huyo ameunda Baraza la Mawaziri bila kuzingatia usawa wa dini na kwamba, kwenye baraza hilo kuna mawaziri wanane tu ambao ni Waislamu.

Amesema kuwa, Rais Magufuli hatakiwi kusikiliza ushauri wenye ukada ndani yake kwani wanaCCM wengi hawana uzalendo na nchi.

Sheikh Ponda amemtaja Benard Membe ambaye alikuwa Waziri Mambo wa Nje katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwa, alimshauri Rais Magufuli njia sahihi ya kutatua mgogoro wa Zanzibar.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza amesema kuwa, Rais Magufuli anafukia shimo kwa kuchimba shimo lingine kutokana na kushindwa kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzaibar.

Amesema kwamba, mgogoro huo hauwezi kutatuliwa kwa kutumia majeshi wala silaha za moto pia kurudia uchaguzi isipokuwa maafikiano.

“Kuvurukiga kwa uchaguzi wa Zanzibar sio suala geni na kwamba kwanini chaguzi za nyuma hazijarudiwa,”amehoji Askofu Bagonza huku akionesha kushangazwa na Rais Magufuli kushindwa kupata ufumbuzi wa mgogoro huo mpaka sasa.

error: Content is protected !!