July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanasiasa watajwa mauji ya albino

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Ame Silima akijibu hoja mballimbali za wizara yake Bungeni

Spread the love

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima, amesema huenda kuna ukweli wa wanasiasa kuhusika na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino). Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Silima amesema viashiria hivyo vya wanasiasa kuhusika vinatokana na kuwepo kwa ongezeko la matukio hayo pale inapofikia kipindi cha uchaguzi wa mkuu wa madiwani, wabunge na rais.

Alitoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), ambaye alitaka kujua ni kwanini serikali na Bunge wamekaa kimya bila kutoa tamko lolote baada ya vyombo vya habari vya ndani na nje kuandika kuwa wanasiasa wanahusika na matukio hayo.

“Ni kwanini serikali na Bunge wamekaa kimya bila kutoa majibu yoyote juu ya taarifa hizo na ni kwanini waandishi hao wasitafutwe ili wakatoa ushahidi wa kuwabaini wanasiasa hao ili wale ambao hawahusiki serikali iweze kuwasafisha.

“Pia serikali ilitangaza kuwa itawapatia albino vifaa maalum kwa ajili ya kuwakinga na majanga ya mauaji ambayo yanawaandama lakini mpaka sasa hakuna juhudi zozote au ndio kusema serikali inashangilia kwa mauaji hayo na ndiyo maana inawadanganya? amehoji Selasini.

Swali Selasini limetokana na swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Philipa Mturano (Chadema), aliyetaka kujua mpaka sasa kuna watu wangapi ambao wamekamatwa na kuthibitishwa na mahakama na wamefanywa nini.

Akijibu maswali hayo, Silima amesema kuwa kuna uwezekano wa wanasiasa kuhusika na mauaji hayo kwani vitendo hivyo huongezeka kutokana na vuguvugu la uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais.

Ameongeza kuwa, hakuna haja yoyote ya kuwatafuta waandishi wa habari juu ya hilo bali cha msingi wanasiasa na wabunge kwa ujumla wanatakiwa kutambua kuwa hakuna ubunge wala nafasi yoyote ambayo inaweza kupatikana kwa kutumia kiungo cha albino.

Silima ameongeza kuwa mpaka sasa watuhumiwa 15 wa mauaji ya albino wamekamatwa na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Mbali na hilo, amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka waganga wa kienyeji ambao wanapiga ramli chonganishi.

Kuhusu vifaa vya kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi, Silima amesema kuwa serikali inaendelea na utaratibu wa kuvihakiki vifaa hivyo kwa usalama wa jamii hiyo.

error: Content is protected !!