July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wanaowabeza Polisi mitandaoni ‘kushughulikiwa’

Spread the love

JESHI la Polisi limefura. Ni kufuatia watu mbalimbali kulibeza mitandaoni kwa madai kuwa, limejikita katika matamko na mazoezi ya kukabili maandamano ya vyama vya siasa vya upinzani, kuliko kujipanga kukabiliana na uhalifu mkubwa ukiwemo ujambazi, anaandika Pendo Omary.

Askari wanne waliuawa katika tukio la ujambazi lililotokea usiku wa jana, eneo la Mbande, Mbagala jijini Dar es Salaam na kuibua maoni tofauti ya wananchi katika kipindi hiki ambacho polisi wamekuwa wakijitokeza mitaani na kufanya maonyesho kwa madai ya kujiweka tayari kuwakabili wahalifu.

Nsato Marijani, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi hapa nchini amewambia wanahabari hii leo kuwa, jeshi hilo halitavumilia ‘ushabikiaji’ wahalifu unaofanywa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii huku wakilibeza jeshi la polisi.

CP Marijani aliwaita wanahabari ili kuzungumzia mazingira ya tukio la kutokea kwa mauaji ya askari wa jeshi hilo siku ya jana, ambapo amesema, kitendo kilichotokea jana sit u ni uhalifu bali ni “tangazo la vita dhidi ya Polisi”.

“Wahalifu walifanikiwa kupora bunduki zetu mbili aina ya SMG na risasi 60 na hawakuchukua pesa wala kuharibu mali yoyote ya benki hiyo. Maana yake wahalifu hao walilenga kuwashambulia askari polisi wetu,” amesema na kusisitiza;

“Inashangaza kuona baadhi ya watu wanashabikia uhalifu kutokea kupitia mitandao ya kijamii na natoa onyo kali kwao, waache kuhamasisha uhalifu maana tunawasaka, tutawakamata na kuwahoji ili sheria ichukue mkondo wake.”

Jeshi hilo limesema, tayari limewakamata baadhi ya watu wakihusishwa na mauaji hayo.

error: Content is protected !!