June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanaoidai Uchumi Supermarket waiangukia serikali

Spread the love

WASAMBAZAJI bidhaa za kampuni mbalimbali zilizokuwa zikifanya kazi na kampuni ya Uchumi Supermarket ya Uchumi wameitaka Serikali kuwasaidia kulipwa madeni wanayoidai kampuni hiyo baada ya kufungwa bila ya kupewa taarifa yanayofikia bil. 4.4. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Kufungwa kwa kampuni hiyo ambayo chimbuko lake ni nchini Kenya kunadaiwa kuwa kunatokana nakufilisika hali iliyopelekea kushindwa kulipa madeni ya wasambazaji hao wakubwa na wadogo.

Wakizungumza na MwanaHALISI Online kwa nyakati tofauti baadhi ya wasambazaji hao ambayo idadi yao 202, wamesema serikali ndio chombo pekee cha kuwasaidia ili kupata haki zao kwani hata wakikaa na ubarozi wa Kenya ambako ndiko kampuni hiyo inatokea, hawataweza kufanya kitu bila ushirikiano wa Serikali.

Mwenyekiti wa muda wa madai ya wasambazaji hao, Joseph Mlay amesema kufungwa kwa Supermarket hiyo bila taarifa hakujaleta picha nzuri ya kibiashara kutokana na hasara iliyosababishwa na tukio hilo.

Mlay ambaye anafanya kazi ya usambazaji wa mabarafu katika Supermarket hiyo amesema tayari hatua za awali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandika barua kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick na Meya wa jiji Didas Masabuli kuwataka kuongeza nguvu ya kutatua tatizo hili kwani wakati wa ufunguzi wakampuni hiyo walikuwepo.

Katibu wa wasambazaji hao ambaye pia ni akaunti meneja wa kampuni ya Chai Bora, Floriana John amesema kampuni yao inaidai Uchumi Supermarket mil. 37 katika kipindi cha miezi miwili ambazo zimepelekea kumeporomoka kwa uchumi na maendeleo yao na uaminifu kwa wateja waliokuwa wakishirikiana nao kutokana na madeni wanayodaiwa.

John amesema katika tukio hilo wengi walioathirika ni wajasiriamali wadogo wanaofanya biashara za mboga mboga kutokana na ugumu mkubwa wanaoupata katika kuandaa biashara zao kutoka mashambani huku kipato chao kikiwa kidogo zaidi.

Naye Msambazaji wa bidhaa za kampuni ya Bidco Oil & Soap ambayo pia inadai Mil. 10 kwa zaidi ya miezi sita sasa, Baraka Sawe amesema madhara makubwa yameikumba kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kukosa soko kutokana na kutegemea soko katika Supermarket ya Uchumi hivyo kupelekea kushindwa kuendesha biashara.

error: Content is protected !!