July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanaochunga kwenye hifadhi waonywa

Ng'ombe wakiwa machungoni

Spread the love

SERIKALI imewaonya na kutishia kuchukua hatua za kisheria kwa wafugaji ambao wanachunga mifugo yao katika hifadhi mbalimbali hapa nchini. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamoodi Mgimwa, amelieleza Bunge alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (Chadema).

Katika swali la msingi la Pareso alitaka kujua ni lini serikali itatatua mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa kata ya Bugeri wilayani Karatu na TANAPA ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa utulivu.

Akijibu swali hilo, Mgimwa amesema kuwa eneo la msitu wa Maranq lilikuwa msitu wa hifadhi tangu mwaka 1957.

Amesema kuwa msitu huo ulipandishwa hadhi na kujumuishwa kwenye sehemu ya hifadhi za taifa za ziwa Manyara kwa tangazo la Serikali Na 105 la mwaka 2009.

Kwa mujibu wa Mgimwa, kabla ya kupandishwa hadhi na kujumuishwa kwenye Hifadhi ya Ziwa Manyara, msitu huo haukuwahi kuwa chini ya kijiji chochote hata hivyo wananchi walikuwa wanaruhusiwa kuingia na kuokota kuni.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa Tanzania sura ya 282 baada ya msitu Marang kupandishwa hadhi, wananchi hawaruhusiwi kufanya shughuli yoyote ikiwemo kuokota kuni.

“Kutokana na hali hiyo, hakuna mgogoro wowote kati ya wananchi wa kata ya Bugeri na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) unaohusiana na eneo la msitu wa Marang,” amesema Mgimwa.

error: Content is protected !!