January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi watofautiana na Kanisa

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alipomkabidhi ofisi, Waziri mpya wa wizara hiyo, William Lukuvi

Spread the love

WANANCHI wa Kijiji cha Mahanji, Kata ya Matamba wilayani Makete mkoa wa Njombe, wameandamana kupinga ardhi ya shamba la kijiji isitwaliwe na Kanisa Katoliki. Anaandika Mwandishi wetu … (endelea).

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Kahawa Nyambo, ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa shamba hilo ni mali ya kijiji ambacho kina utaratibu wa kuwagawia wananchi pamoja na taasisi mbalimbali likiwemo kanisa kwa ajili ya kilimo cha mazao ya muda mfupi.

“Upandaji wa miti ulioanza kufanywa na kanisa katika shamba hilo, ndio umewashtua wananchi na hivyo wakaamua kuandamana kudai miti iondolewe kwenye shamba lao,” amesema Nyambo.

Mmoja wa waandamanaji hao aliyejulikana kwa jina moja la Chepe, amesema kuwa mashamba hayo hayajauzwa kwa mtu yeyote na kwamba kilichofanywa na kanisa ni kinyume cha makubaliano ya matumizi ya ardhi hiyo.

Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Matamba, Padre Albert Mligo, amesema kanisa lilipewa eneo hilo la shamba tangu mwaka 1980 na kwamba wamekuwa wakitumia ardhi hiyo kwa kipindi chote hicho kama mali yao.

“Sasa tumeamua kupanda miti kama moja ya miradi inayotekelezwa na kanisa,” alisema padre Mligo.

Kamati ya watu 18 tayari imeundwa ikiwashirikisha serikali ya kijiji, kanisa na wananchi ili kusuluhisha mgogoro huo,ambapo vikao vinaendelea kwa ajili ya kuumaliza. Kamati italeta majibu ya muafaka 11 Mei, mwaka huu.

Kijiji cha Mahanji ni miongoni mwa vijiji vitano katika wilaya ya Makete vinavyoongozwa na Chadema baada ya kupata ushindi kubwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

error: Content is protected !!