November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi watoa ya moyoni bajeti 2019/20

Bajeti mwaka 2019

Spread the love

BAADHI ya wananchi waliotoa maoni kuhusu mapendekezo ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 mkoani Kagera na Dodoma, wamekuwa na maoni tofauti. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Julius Kato, Mkazi wa Manispaa ya Bukoba leo tarehe 14 Juni 2019 amesema, bado kuna mambo ambayo yanakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi, kwa kuwa vitu vingi vimekuwa vile vile na kodi ni zile zile hivyo hakuna unafuu wowote.

Amesema, kama serikali ikitaka kuweka vizuri suala la bajeti, iangalie kwa haraka masuala ambayo yanamlenga mwanachi wa kawaida na wa chini huku akisisitiza kuwa, bajeti hii ni kama ya wafanya biashara tu.

Eustace Kazimoto, Mkazi wa Kata ya Kalabagaine, Bukoba vijijini amesema kuwa, watu wa vijijini wamekuwa na ugumu kuielewa bajeti na ndio maana kila mara wanashtukia vitu vimepanda bei.

Emiliana Kaiza, Mkazi wa Kashai na mfanyabiashara Manispaa ya Bukoba amesema kuwa, bajeti ni nzuri kwani kuna mambo mengi yatakuwa nafuu kwa wafanyabishara hivyo yatawafanya wafanye kazi kwa uraisi, bila kusumbuliwa na watalipa kodi kwa wakati, bila tatizo.

Wakazi wa Dodoma, Rachel Chibwete na Jamila Badweli kwa pamoja wamesema kuwa, kiwango cha kodi ya katika nywele bandia ni kidogo na kilitakiwa kuongezwa.

Naye Dastani Ngonyanyi ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Uunguzi Milembe amesema kuwa, kitendo cha kuongeza kodi katika nywele za bandia ni kuwanyima uwezo akina dada kujipamba.

Dar es Salaam, Alex Justin wa Kinondoni jijini Dar es Salaam amesema kuwa, hajui chochote kuhusu bajeti hiyo iliyosomwa jana nchini.

“Sijajua chochote, mie sikufuatilia jana kwa kuwa nilikuwa na mambo yangu mwenyewe,” amesema.

Salma Ramadhan wa Sinza, Ubungo amesema kuwa, kikubwa alichokielewa kwenye bajeti hiyo, ni serikali kujaribu kujenga mazingira mazuri kwa wafanyabiashara huku wafanyakazi wakiwekwa kando.

“Serikali imeangalia namna ya kuwabeba wafanyabiashara kwenye bajeti hii, hiki ni kitu kizuri,” amesema.
error: Content is protected !!