July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi watifuana na polisi Mwanza

Spread the love

POLISI jijini Mwanza wamewatawanya wananchi kwa mabomu katika eneo la Sinai, Mtaa wa Nyerere ‘A’ Kata ya Mabatini baada ya kutokea vurugu kutokana na mtu mmoja kugongwa na gari, anaandika Moses Mseti.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu hao wakati wakimuokoa dereva wa gari namba T. 520 CBM Mark X, Lifaty Dickson ambaye alimgonga mtoto wa miaka sita, Festo William.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya wananchi kuhisi kwamba polisi walitaka kumtorosha dereva huyo kwa madai ya kufanya ajali bila kukusudia.

Wananchi wanadai dereva huyo alifanya ajali baada ya kuendesha kwa mwendo kasi na hatimaye kumgonga na kumsababishia mauti motto huyo aliyekuwa Mkazi wa Kata ya Mahina.

“Mimi nilikuwa katika eneo hili la ajali ilipotokea, sasa huyu mtoto aliyefariki (Festo William) alikuwa anavuka katika eneo la watembea kwa miguu, zebra lakini huyu mwenye gari alishindwa kupunguza mwendo.

“Baada kuona hivyo sisi kama wananchi wapenda haki tulianza kumuadabishi huyu mtu lakini polisi wakaingilia kati na sisi hatukukubali, “amesema shuhuda mmoja aliyetambulika kwa jina la Simon.

Justus Kamugisha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kumuokoa dereva wa gari hilo ambaye alikuwa akishambuliwa na wananchi.

Kamugisha amesema kuwa, polisi wake walishambuliwa kwa kupigwa mawe na wananchi hao, hivyo hawakuwa na njia yeyote ya kujiokoa tofauti na kutumia mabomu ya machozi.

“Polisi hawakuwa na njia yoyote tofauti na hiyo, waliamua kufanya hivyo ili kumuokoa dereva wa gari hilo na kuokoa raia wema wengine,” amesema Kamugisha na kuongesha kuwa watu watatu wanashikiliwa na polisi kutokana na mkasa huo.

error: Content is protected !!