July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi watakiwa kutunza ardhioevu

Spread the love

WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Kitengo cha Ardhioevu, imewataka wananchi hususan waishio kwenye maeneo yenye ardhioevu kwa kudhibiti ongezeko la shughuli za kimaendeleo. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Miongoni mwa shughuli wanazopaswa kudhibitiwa ni pamoja na ujenzi kwenye vyanzo vya maji, ufugaji holela, kilimo kisichozingatia kanuni na kukata miti ovyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Ofisa Wanyamapori na Uhifadhi Ardhioevu, Sadiki Lotha Laisser “Ardhioevu uhifadhi ndegemaji mfano taji, korongo nyangumi bungunusu, heroe mdogo na mkubwa.

“Ndege hawa ni muhimu kwa utalii na uhifadhi wa mazingira pamoja na mwingiliano wa bionuawi. Pia ni dalili na kiashiria cha afya ya mazingira,” amesema Laisser.

Laisser amesema kuwa, kila mwaka tarehe 2 Februari huadhimishwa siku ya ardhioevu duniani ili kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa utunzwaji wa ardhi hiyo na faida zake kwa maendeleo ya jamii.

Amesema kauli mbiu ya siku ya maadhimisho ya ardhioevu mwaka huu ni ‘Maisha ya Kipato Endelevu’ ujumbe huu umelenga kuwahamasisha wananchi kuwa, wanatakiwa kujipatia kipato katika hali endelevu. Pia kutumia rasilimali za asili kwa kuzingatia masilahi ya vizazi vijavyo.

“Wananchi waishio kwenye maeneo yaliyo karibu na ardhioevu wanatakiwa kutumia rasilimali za asili kwa kuzingatia kuwa vizazi vijavyo pia vitahitaji rasilimali hizo.

“Watumie kilimo rafiki, mifugo ya kiasi yenye tija, uvuvi wenye kuzingatia kanuni, majengo yajengwe kwenye maeneo stahiki na viwanda kutomwaga maji machafu kwenye vyanzo vya maji kabla ya kuyatibu wala kutupa taka ngumu,” amesema.

Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya ardhi ya Tanzania ni ardhioevu ambayo ni muhimu kwa kukuza uchumi, bionuwai, shughuli za kijamii na kiikolojia.

Maeneo hayo ni makazi muhimu ya aina tofauti za viumbe hai wakiwemo samaki, ndege, viboko, mamba na wengine wasio na uti wa mgongo.

Vilevile maeneo hayo ni muhimu kwa kuchuja kemikali zilizopo kwenye maji yaliyochafuka yatokayo kwenye kilimo, viwanda na matumizi ya nyumbani na madini ya Nitrojeni na Phosphorus ambayo yakizidi husababisha maji kuoza na kupungua kwa hewa muhimu ya oxygen kwa viumbe wa majini.

Mkuu wa Ofisa Idara ya Wanyamapori nchini, Pellage Kauzeni amesema kuwa tarehe 13 Februari mwaka huu, itakuwa siku ya kuhesabu ndege waishio kwenye ardhioevu ili kupata takwimu sahihi ya ndege waishio kwenye ardhi hiyo.

“Tarehe 13 Februari mwaka huu itakuwa siku ya kuhesabu ndege waishio kwenye ardhioevu nchi nzima kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa masuala hayo na wahitimu kadhaa kutoka Chuo cha UDSM na Sokoine,” amesema.

Kauzeni amewakumbusha wananchi wote kuwa maeneo ya ardhioevu siyo ardhi bilashi bali ni maeneo muhimu kwa maisha ya kila siku hivyo haina budi kutunzwa kwani yakitoweka hayatarudi tena.

Wizara inawashauri wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya ardhioevu kushirikiana na serikali katika kuyatunza maeneo hayo. Pia wanakumbushwa kuwa maeneo ya ardhioevu ndiyo vyanzo vya maji ambayo binadamu wanatumia kila siku sambamba na wanyama na mimea.

error: Content is protected !!