May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi watakiwa kujiandaa wimbi la nne Korona, wasisahau tiba asili

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Said

Spread the love

 

WATANZANIA wametakiwa kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na mlipuko wa Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), ili kudhibiti athari zake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumamosi, tarehe 7 Agosti 2021 na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimemti ya Maafa, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Said, akifungua warsha ya kuwajengea uwezo watetezi wa haki za binadamu katika kukabiliana na maafa na majanga, mkoani Dar es Salaam.

Warsha hiyo imeandaliwa na Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Kanali Said amesema kuwa, wananchi hawapaswi kubweteka kwa kuacha kufuata miongozo inayotolewa na wataalamu wa afya, kwa sababu waliweza fanikiwa kubaki salama katika mawimbi matatu ya mlipuko wa Korona, kwani wimbi la nne la janga hilo liko njiani.

Amesema ni bora wananchi wakachukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo, ili kuepuka kupata maambukizi yake, kwa kuwa tiba yake ni gharama, hasa inapofikia wakati mgonjwa anatakiwa kupata msaada wa kupumua kupitia mashine ya Oksijeni.

“Tusione tulishinda mwanzo tukatembea kusema mimi nilishinda ya kwanza nitapona,  hapana sasa dunia iko katika wimbi la tatu,  tunasikia la nne liko njiani likitukuta tuna elimu ya kutosha kuzuia na kuchukua hatua,  jamii ya Watanzania itakuwa salama,” amesema Kanali Said.

Kanali Said amehimiza wananchi waendelee kufuata njia zilizotumika kukabiliana na wimbi la kwanza na UVIKO-19, ikiwemo kutumia tiba asili.

“Huwezi ukafika hatua ya kuteseka katika stage (hatua) ya oksijeni. Tunaona miongozo iko vizuri lakini kutokana na jamii kutoelimishwa vya kutosha, inaweza ikaleta shida. Elimu ya mwanzo iendelee,” amesema Kanali Said.

Kanali Saidi ameongeza ” tusiache kunywa chai za tangawizi ili  huyu jamaa asipate sababu za kukusumbua,  watu tulikunywa matangawizi mpaka malimao yaliisha, ilifika kipindi watu walitubeza. Tulipunguza maambukizi tukaona tumevuka pale,  kumbe inatakiwa tuwe na utaratibu wa hivyo”

Kanali Said amewahimiza wananchi wapate chanjo ya Korona ili wawe salama.

“Usisubiri vinavyotengenzwa kwa kemikali pekee yake  wakati tiba asili ipo,  bado tiba asili inasisitizwa. Mtu mmoja mmoja achukue hatua,  chanjo imekuja tuchukue fursa tupige tuwe salama,” amesema Kanali Said.

Kanali Said amesema idara yake imejipanga vizuri kukabiliana na janga hilo, huku akizitaka asasi za kiraia na makundi mbalimbali kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya janga hilo.

error: Content is protected !!