July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi wataka chombo huru usimamizi Hifadhi ya Ngorongoro

Spread the love

 

KAMATI ya kutafuta suluhu za mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro nchini Tanzania imeshauri kiundwe chombo maalumu kitakachosimamia, ratibu na kudhibiti matumizi ya ardhi, uhifadhi wa kiikolojia hifadhini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Manyara … (endelea).

Pendekezo hilo, pamoja na mapendekezo mengine, yaliwasilishwa na kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai, mwishoni mwa wiki kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, jijini Dodoma.

“Chombo lazima kiwe na wajumbe 10, watano kati yake watoke katika jamii na watano watoke katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA),” yanaeleza mapendekezo hayo.

Kuhusu changamoto ya ongezeko la watu, kamati hiyo imependekeza watu waondoke hifadhini humo kwa hiari bila ya kushinikizwa kwa vitisho, kunyimwa huduma za kijamii.

“Mchakato wa uhamishaji lazima ubadilishwe, ujumuishe na ufuate kibali chao cha bure,” imeeleza taarifa ya kamati hiyo.

Serikali ya Tanzania, imetenga eneo wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, kwa ajili ya wananchi wa Ngorongoro wanaotaka kuhama hifadhini humo kwa hiari, ambapo imejenga nyumba zaidi ya 300 kwa ajili yao.

Kamti hiyo imependekeza idadi ya vyombo vya usafiri, ikiwemo magari vinavyoingizwa katika bonde la Ngorongoro, ipunguzwe ikishauri kwa siku yaruhusiwe magari 50 kuingia hifadhini humo, ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Pia, imeshauri idadi ya nyumba za malazi kwa watalii ipunguzwe ili kupunguza wingi wa majengo yasiyokuwa na sababu.

Mgororo huo wa ardhi umeibuka kufuatia madai ya ongezeko la idadi ya watu, mifugo na shughuli za kibinadamu, linaotishia usalama wa hifadhi hiyo.

error: Content is protected !!