August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi wasaka viwanja Dodoma

Spread the love

DHAMIRA ya Rais John Magufuli ya kuhakikisha Dodoma inakuwa Makao Makuu ya Nchi imechochea wananchi kuanza kutafuta viwanja katika mji huo, anaandika Drfany Tibason.

Wananchi wa Dodoma na nje ya mji huo wameanza kusaka viwanja na wengine wakishawishi baadhi ya watu wenye uwezo mdogo kuhakikisha wanaviendeleza ili vibaki mikononi mwao.

Mmoja wa wakazi ambao wametembelewa na madalali ambaye alijitambulisha kwa jina la Mdala Emmy amesema, kwa muda mfupi ametembelewa na zaidi ya watu saba wakimtaka awauzie kiwanja chake.

“Nimekaa miaka mingi sijawahi kutembelewa na watu kwa ajili ya kuuza kiwanja changu lakini siwezi kuuza kwani wapo wajukuu wangu watakuja kujenga hapo baadaye.

“Ni kweli siwezi kujenga, mjukuu wangu si unaona hali yangu lakini nina wajukuu ambao baba yao aliwaacha hivyo watajenga wenyewe ikifika wakati wao wa kujenga, kwa sasa wanasona” amesema Mdala Emmy.

Alhajj Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma hivi karibuni aliziagiza halmashauri zote kuhakikisha zinapata viwanja katika Mji wa Dodoma kama sehemu ya kitega uchumi.

Alhajj Kimbisa amewaagiza wakurugenzi kuhakikisha wanafanya mawasiliano na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ajili ya kuomba viwanja ambavyo vinaweza kutumika kama sehemu ya kitega uchumi.

“Kila mtu anajua muda si mrefu Dodoma inakuwa Makao Makuu hivyo basi CCM Mkoa wa Dodoma imewaelekeza wakurugenzi wote wa wilaya wahakikishe wanapata viwanja mjini Dodoma.

“Viwanja hivyo vinaweza kutumika kama kitega uchumi, wakishapata viwanja hivyo wanaweza kuvitengenezea hati ambayo itasaidia kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali na kuzifanya halmashauri hizo.

“Mnajua kwamba kwa sasa wilaya zote zinatakiwa kujitegemea hivyo ni vyema mkachangamkia fursa ya kupata viwanja ili kuweza kufanya mambo ya maendeleo kwa manufaa ya halmashauri husika pamoja na wananchi wake” amesema.

Pia CCM Mkoa wa Dodoma imesema, imapongeza kauli ya Rais John Magufuli kutaka Dodoma kuwa Makao Makuu.

Amesema, Dodoma kuwa Makao Makuu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2015-2020 ibara ya 151(a),(b).

error: Content is protected !!