August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi waomba ufafanuzi maliasili

Spread the love

WANANCHI waishio jirani na hifadhi za wanyama wilayani Ulanga, Morogoro wameiomba serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuwapa ufafanuzi wa kupata fidia pale wanyama pori wanapoingia kwenye mashambani yao na kuharibu mazao, anaandika Christina Haule.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi hao akiwemo Christina Samwel wamesema kuwa, wanalazimika kuomba ufafanuzi kutokana na wanyama wakiwemo Tembo kuingia kwenye mashamba yao na kuharibu mazao ya chakula hivyo kuwasababishia hasara.

Samweli amesema, kufuatia Tembo kufika kwenye mashamba yao mara kwa mara, wamekuwa wakiingiwa hofu ya usalama wa maisha yao mbali na kuharibiwa mazao yao.

Bakari Rashidi ambaye ni mkazi wa Ulanga amelalamikia kitendo hicho akisema kuwa, wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao yao huku na kusababisha kukosa chakula pia fidia.

Frances Kauzeni, mratibu wa mradi wa kusimamia rasilimali za misitu Kilowemp, Ulanga amesema, katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero hiyo ya wanyama waharibifu, Wizara ya Maliasili kupitia mradi wa Kilowemp wamekuwa wakitoa elimu juu ya kuepuka wanyama waharibifu na kutunza mazingira ili rasilimali hizo ziwanunufaishe.

Amesema kuwa, asilimia kubwa ya wakazi wa maeneo hayo tayari wamepatiwa elimu hiyo na amewaomba kuitumia ili kuweza kutunza maliasili hizo sambamba na mazao yao.

Awali Dk.  Stephen Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameuagiza uongozi wa wilaya na vijiji kuhakikisha hakutokeai uvamizi wowote wa ardhi unaolenga kuharibu mazingira kwa kuingiza mifugo kupita kiasi kwenye maeneo yote ya hifadhi na mapori tengefu.

Amesema, suala la kuruhusu uvamizi wa ardhi katika maeneo mbalimbali hasa yaliyotengwa, unaweza kuwa sababu kubwa ya uharibifu wa maliasili na hata wanyama kuingia kwenye makazi ya watu na kuharibu mazao yao.

error: Content is protected !!