August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi wamshutumu mbunge wa Ilemela

Spread the love

ANGELINA Mabula, Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza, analalamikiwa na Wananchi wa Mtaa wa Nyanguku na Lukobe uliopo katika Kata ya Kahama kwa kushindwa kuwasaidia kulipwa fidia za ardhi yao, anaandika Moses Mseti.

Wananchi hao wapatao 6000, wanamlalamikia mbunge huyo kutokana na maeneo yao yenye ukubwa wa zaidi ya hekta saba kuchukuliwa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani humo bila fidia.

Akizungumza hivi karibuni, katika kikao cha kujadili kuhusu kuchukuliwa maeneo yao, Paulo Lameck, Mwenyekiti wa Mtaa wa Lukobe amesema kuwa, malalamiko na lawama zote wanamtupia Mabula kwa kushindwa kuwasaidia.

Lameck amesema kuwa, wanamtupia lawama mbunge huyo kutokana na kushindwa kuwasaidia, kuzungumza na wahusika wanaodaiwa kuchukua maeneo hayo kitendo ambacho kimesababisha waendelee kuishi kama wakimbizi katika nchi yao.

“Tangu mwaka 1960 tunaishi hapa, Novemba 2006 ndio tuliambiwa kwamba tunapaswa kuondoka katika maeneo haya, kwa madai siyo ya kwetu, sasa nashangaa miaka yote hiyo babu na baba zetu wameishi hapa 2006 ndio tuhamishwe,” amesema Lameck.

Amesema, baada ya hali hiyo kuzidi kuwa tete kufuatia nyumba zao kubomolewa nyakati za usiku na watu wasiofahamika, Machi 2015 waliamua kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kutoa kilio chao.

Lameck amesema, baada ya kutoa kilio hicho katika Wizara ya Ardhi, Juni mwaka 2015, watalaamu wa wizara hiyo walikwenda katika maeneo yao na kufanya tathmini lakini mpaka sasa bado hawafahamu hatma yao.

“Machi 2016 tulikwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, (Manju Msambya) lakini na yeye hakuweza kutusaidia na baada ya kuona hatupati msaada, tukaandika barua kwenda kwa Waziri wa Ardhi (William Lukuvi) na mpaka sasa hakuna majibu,” amesema Lameck.

Benard Mkina, Diwani wa Kata ya Kahama, amesema kuwa, wananchi wake wanateseka na kwamba wengine wamepoteza maisha kutokana na kunyang`anywa maeneo yao na kuwa, watu waliyoyachukua kwa sasa wanachimba mchanga na kuuza.

Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi alipotafutwa na mtandao huu kupitia simu yake ya mkononi kuzungumzia malalamiko hayo, alijibu “nipo kwenye kikao na kukata simu.”

Kheri James, Katibu wa mbunge alikiri kuwepo kwa suala hilo huku akiwatupia lawama John Wanga, Mkurugenzi wa Ilemela na Manju Msambya, aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

“Hilo suala tunalifahamu na sisi kama ofisi ya mbunge tuliishalifuatilia na mamlaka husika waliahidi kulifanyia kazi.

“… lakini mkurugenzi (John Wanga) na watu wake wanameshindwa kufanya majukumu yao wanataka sisi tuyafanye,” amesema James.

error: Content is protected !!