MATOKEO ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya TWAWEZA kati ya tarehe 18 Juni na 12 Julai 2022 kwa wahojiwa 3,000 waliopigiwa simu, yameonesha asilimia 68 ya wananchi wamefurahishwa na maboresho ya huduma za jamii katika kipindi cha miezi sita iliyopita, hasa sekta ya elimu. Anaripoti Felister Mwaipeta, TUDARCo … (endelea).
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa leo tarehe 25 Agosti, 2022 pia asilimia 60 wamesema uhuru wa kujieleza umeboreshwa, asilimia 56 wamesema uhuru wa kisiasa umeimarika, asilimia 59 wamesema ulinzi na usalama na kupungua kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake (61%) na watoto (60%).
Hata hivyo, asilimia 68 ya wananchi wamesema gharama za maisha zimepanda zaidi katika kipindi hicho, na 48 wamesema upatikanaji wa ajira na fursa za kujipatia riziki za maisha vimepungua badala ya kuongezeka.
“Kwa ujumla, wananchi wengi wanasema nchi iko kwenye mwelekeo sahihi (30%) wachache wanasema nchi haiko kwenye mwelekeo sahihi (25%), ingawa wengi zaidi (44%) wana hali ya sintofahamu kuhusu mwelekeo wa nchi. Matumaini ya wananchi kuhusu suala la uchumi yako chini sana. Idadi ya wanaosema hali ya uchumi ni mbaya ni mara nne (41%) ya wale wanaosema uchumi ni mzuri (9%),” imesema ripoti hiyo.
Leave a comment