July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi wamkaba Magufuli kwa ahadi zake

Spread the love

BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma wametoa maoni yao kwa kumtaka Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati akiomba kura. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Kwa upande wake mwanachi wa wilaya ya Mpwapwa, Hawa Makau amesema kuna kila sababu rais kuhakikisha anatoa kipaumbele zaidi kwa watumishi hasa katika sekta ya elimu.

Amesema ni ahadi nyingi ambazo zilitolewa wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na elimu bure lakini bila kufafanua kuwa elimu hiyo itatolewaje kama hakuna uboreshaji wa maisha ya watumishi.

Mbali na hilo amesema sekta ya afya ni tatizo kubwa na sugu licha ya kwamba wapo watu ambao wana bima za afya lakini upatikanaji wa dawa bado ni mtihani mkubwa.

“Tumekuwa kutihamasishwa kukata bima ya afya lakini cha kushangaza ukienda katika hospitali za wilaya unaambiwa hakuna dawa na unaelekezwa sehemu ya kununua jambo ambalo linazua utata mkubwa na kujiuliza nini maana ya kuwa na kadi hiyo.

“Kutokana na hali hiyo ni bora sekta ya afya ikapewa kipaumbele zaidi kwani bila kuwepo na afya bora hakuna uzalishaji ambao unaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Taifa haliwezi kuendelea kama lina watu ambao wana afya mbovu hivyo ahadi za rais wa awamu ya tano aachane na propaganda za kisiasa na badala yake afanye kazi kwa faida ya watanzania na siyo kwa faida ya kikundi cha watu wachache,” amesema Hawa.

Naye mmoja wa walimu ambaye hakutaka jina lake litajwe katika gazetini, amesema haiwezekani serikali ikatangaza elimu bure kama walimu hawataboreshewa maisha yao na kuwekewa mazingira rafiki ya kazi.

Amesema elimu ya Tanzania siyo mbaya ila inaonekana kuwa mbaya kutokana na serikali kutoweka utaratibu wa kuboresha maisha ya walimu pamoja na mazingira mazuri ya kazi.

“Haiwezekani mwalimu akawa anakalia jiwe na mwanafunzi anakalia jiwe, kama haitoshi walimu wanafikia hatua ya kuchangishana hela kwa ajili ya kununua chaki hapo elimu inaweza kuwa bure kweli.

“Hata kama watasema elimu bure bila kuboresha maisha ya mwalimu na mazingira yake ni kazi bure ikumbukwe kuwa mpaka sasa kuna michango mingi ambayo ni zaidi ya kulipa ada,” amesema mwalimu huyo.

Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la EAGT Siloam Ipagara, Evance Lucas amemtaka rais wa awamu ya tano, Dk. Magufuli kuhakikisha anawaunganisha watanzania na kuwa kitu kimoja.

Amesema kwa sasa kipindi cha uchaguzi kimeisha hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwepo kwa makundi au kufanya chuki za aina yoyote bali kinachotakiwa ni watanzania kuwa wamoja.

“Nchi hii ni yetu wote hatuwezi kubaguana kwa rangi, dini, kabila wala ukanda na wala hakuna sababu yoyote ya kujengeana chuki kinachotakiwa ni kuhakikisha watanzania wanaunganishwa na kuwa kitu kimoja kwa faida ya taifa la Tanzania,” amesema Mchungaji Evance.

Akizungumzia juu ya vipaumbele alivyovitoa Rais wakati wa kampeni amesema ni vingi, lakini ni lazima atekeleze ushushaji wa bei ya vifaa vya ujenzi.

Mchungaji Evance amesema jambo pekee ni viongozi wa dini kuendeleza maombi ili mungu aiwezeshe amani nchi ya Tanzania.

error: Content is protected !!