January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi wamgomea Mgombea Urais, ahairisha mkutano

Spread the love

MGOMBEA Urais Kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashimu Rungwe jana alishindwa kufanya mkutano wake wa kampeni mjini Dodoma baada ya kukosa watu wa kuwahutubia. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Akizungumzia tukio hilo Makamu Mwenyekiti Taifa Chaumma na Mgombea Ubunge wa jimbo la Dodoma Mjini, Kayumbo Kabutali alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la kushindwa kufanya mkutano wao wa kampeni kutokana na maandalizi mabovu na mwamko mdogo wa chama hicho kwa wakazi wa Dodoma.

“Ni kweli ratiba ya Tume ya Taifa inaonyesha tulikuwa tufanye mkutano wetu leo hapa mjini katika eneo la Chang’ombe lakini tumeshindwa kufanya mkutano hapakuwa na watu kabisa ndio maana tukakwama mkutano kufanya,” amesema.

Kabutali amesema yeye hakuwepo Dodoma alikuwa akizunguka mikoani kumnadi Mgombea wao Urais kupitia Chama chao kwa kipindi kirefu hivyo walimwachia jukumu hilo mmoja wa viongozi wao wa Mkoa kuandaa mkutano jambo ambalo hakulifanya.

Amesema walifika eneo walilotakiwa kufanya mkutano akiwa amefuatana na Mgombea wao wa Urais Rungwe lakini hawakukuta mtu yeyote katika eneo hilo na hivyo kuahirisha mkutano.

Aidha amesema sababu zingine zilizochangia kutokuwepo kwa watu kwenye mkutano wao ni kucheleweshwa kufanyika matangazo mitaani kuhusu uwepo wa mkutano wao wa kampeni eneo hilo.

Kwa upande wake Mgombea Urais, Rungwe amesema wameshindwa kufanya mkutano kutokana na mmoja wa viongozi wa chama hicho kupata msiba.

Rungwe amesema hakatishwi tamaa na matukio madogo madogo yanayojitokeza ila ataendelea na kampeni zake mkoani hapa katika maeneo yaliyobaki.

Amesema wameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa 12 mpaka sasa na wanaendelea kuzunguka kufanya mikutano zaidi ya kampeni katika mikoa iliyobaki.

“Hatuna fedha lakini tangu mwanzo tulijipanga kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni, tutatumia usafiri wa mabasi na maeneo mengine hata boda boda ili kuwafikia wananchi.

Amesema kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, chama hicho wakimaliza kampeni mkoani hapa watakwenda mikoa ya Morogoro, Tanga na kuendelea Kilimanjaro hadi wamalize mikoa yote iliyobaki

Rungwe ndiye mgombea pekee wa urais ambaye anajichanganya kwa kufanya kampeni zake kwa kutumia usafiri wa mabasi, pikipiki, gari aina ya Toyota Noah na kutembea kwa miguu umbali mrefu.

error: Content is protected !!