RAIS John Magufuli amesema hatoipa kipaumbele wilaya ya Chato iliyoko mkoani Geita, katika utekelezaji wa miradi ya maji, kutokana na baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kuharibu miundombinu ya maji hasa mabomba. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Septemba, 2018 wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Lamadi kilichopo kwenye jimbo la Busega mkoani Simiyu.
Amesema baadhi ya wananchi wa Chato wamekuwa wakichukua mabomba ya maji na kuyatumia katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji, na kwamba hatopeleka miradi ya maji wilayani humo alikozaliwa ili wajifunze athari za kuharibu miradi ya maji.
“…Wengine wakachukua yale mabomba wakafanya ya umwagiliaji, tuliyaharibu wenyewe, ndio maana katika miradi hii sikutaka ianzie Chato, ili kusudi Chato ijifunze athari za kuharibu miradi ya maji. Ningeanzia Chato nilikozaliwa lakini nimeanzia huku. Nataka Busega muitunze miradi ya maji,” amesema.
Aidha, Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi hasa wakazi wa Busega kwamba wakiharibu miradi ya maji inayotekelezwa jimboni humo, serikali yake haitopeleka miradi mingine.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa kuwachukulia hatua watendaji wa wizara yake wanaofanya ubadhirifu katika ujenzi wa miradi ya maji.
“…Watendaji wengi wa wizara ya maji hawaisimamii vizuri, miradi haikamiliki, ndiyo maana nimekuweka huko, wale watendaji wa maji wasiofanya vizuri nenda ukawashughulikie, miradi mingine wamekuwa wakiichezea, wengine wamekuwa wakiweka wakandarasi wao na kupata pasenti, Katibu Mkuu nenda ukawabane watendaji wa maji,” amesema.
Leave a comment