August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi Sirorisimba wampigia goti JPM

Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

WANANCHI wa Kijiji cha Sirorisimba kilichopo katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati na kufuta milki ya ardhi ya kijiji hicho aliyomilikishwa Ibrahim Chacha Nchama kwa kuwa, umiliki huo hauna baraka zao. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Ibrahim Mniko, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sirorisimba akizungumza na mtandao huu kwa niaba ya wananchi kijiji hicho jijini humo amesema, Nchama alikimilikishwa ardhi hiyo kwa hila.

Amesema, mwenyekiti wa zamani wa serikali ya kijiji hicho (Gisey Gisey) akishirikiana na waliokuwa maofisa watendaji wa wakati huo (Juma Kitulang’ombe na David Mwita) kwa nyakati tofauti pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ardhi ya kijiji walifanya hujuma.

Amedai kuwa, viongozi hao walikula njama na kubariki Nchama amilikishwe ardhi hiyo (shamba namba 127) wakitumia kikao cha dharura cha Serikali ya Kijiji cha Sirorisimba cha Machi 17, 1994 badala ya wananchi wenyewe kuamua kupitia mkutano mkuu wa hadhara kwa mujibu wa taratibu.

“Huu mgogoro umedumu kwa zaidi ya miaka 15 bila ufumbuzi na hatua ulipofikia sasa unahitaji uamuzi wa Rais John Magufuli ili wananchi wapate haki na kuendeleza ardhi yao, maana watendaji wa Wizara ya

Ardhi na Maendeleo ya Makazi , mkoa na wilaya wanaonekana kumbemba mwekezaji huyo (Nchama).
“Suala liko wazi kuwa mkutano wa hadhara wa kijiji ndio wenye mamlaka na si serikali ya kijiji,” amesema Mniko.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa, mtangulizi wake Gisey Gisey akishirikiana na Ofisa Mtendaji wa wakati huo (David Mwita) walikula njama za kuchukua ardhi ya kijiji na kumpa mwekezaji bila wananchi kushirikishwa.

Na kwamba, hakufuata taratibu na baada ya kubaini Nchama alishirikiana na viongozi wa zamani wa kijiji ambapo walimwita kutoa maelezo kwenye mkutano wa kijiji ambao ni wenye uamuzi, alikaidi ndipo wakalazimika kulalamika kwa uongozi wa wilaya, mkoa na wizara bila mafanikio jambo linalowasukuma kwenda Ikulu.

Mniko alieleza kuwa mwenyekiti wa zamani huyo (Gisey) alipoulizwa kuhusu kuvamiwa kwa mashamba ya wananchi, alikiri kujadiliana na mtendaji na kukubaliana kwamba, Nchama apewe ekari 50 kwa makubaliano ya kujenga zahanati kutokana kijiji hicho kukabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za afya.

Kwamba mwekezaji huyo (Nchama) alipewa masharti ya kujenga zahanati ndipo akabidhiwe shamba hilo lakini hadi sasa hakuna zahanati iliyojengwa isipokuwa nyumba ya kudumu ya familia yake ikiwa ni pamoja na kujiongezea ekari 1,950 kutoka 50.

Mniko alionesha masikitiko yake kuwa, wakati mgogoro haujapatiwa ufumbuzi wameshangaa milki ya ardhi inayolalamikiwa kuhamishwa kwenda kwa Kampuni ya Mathayosons Enterprises Ltd ya Musoma badala ya Ibrahim Chacha Nchama anayedaiwa kumilikilishwa bila kufutwa taratibu.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo alieleza zaidi kuwa Machi 17, 1994 uliitishwa mkutano wa dharura wa Serikali ya Kijiji cha Sirori Simba kujadili maombi mbalimbali ya ardhi na kuhudhuriwa na wajumbe 19 kati ya 22.

Lakini muhtasari huo unaodaiwa kutumika kummilikisha Nchama ardhi hauna saini za wajumbe bali za mwenyekiti kijiji Gisey Gisey na mtendaji Juma Kitulang’ombe.

Naye Dorica Kitamara, mjumbe wa serikali ya kijiji kwenye kikao hicho amesema kuwa, walikubali agenda namba 8 ya ujenzi wa zahanati na kilimo katika shamba hilo lenye mgogoro kuwa mwekezaji apewe ekari 50 lakini baada ya wananchi wenyewe kuridhia na si kwa ridhaa na matakwa ya uongozi wa kijiji.

Pia katika hali inayotia shaka kuwa, kuna mchezo mchafu unafanyika mtendaji wa kijiji hicho Isamuhyo Waisaka Agosti 3, mwaka huu alimwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Butiama akidai wananchi walikiri kwenye mkutano wa Mei 25, mwaka huu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati huo Magesa Mulongo kuwa, umiliki wa ardhi hiyo ulifanyika kihalali na taratibu zilifuatwa wakati si kweli.

Inadaiwa kuwa, Februari 27, 1994 Nchama aliomba ardhi ya ukubwa wa ekari 500 za eneo la Kirienyi kwa ajili ya kufuga, kilimo na kupanda msitu wa miti ya mbao na tarehe hiyo hiyo aliomba ardhi (viwanja viwili vikubwa) vya kujenga zahanati, nyumba ya biashara pamoja na nyumba ya makazi akirejea tangazo namba 2 la serikali ya kijiji hicho la Januari 15, 1994 lenye kumb Na. MR/MVS/T14/94/ VOL I.

Akizungumza kwa simu na mtandao huu mwenyekiti wa zamani wa kijiji hicho Gisey Gisey anayeadaiwa kuridhia ardhi hiyo apewe mwekezaji alikiri, lakini akadai kuwa mkutano mkuu wa kijiji ulifanyika na wananchi wakaridhia huku akidai hakumbuki ulifanyika lini.

Hata hivyo, baada ya mtandao huu kumtajia mkutano wa dharura wa serikali ya kijiji pekee wa Machi 17,1994 ndio ulitumika kummilikisha ardhi mwekezaji na hakuna mjumbe hata mmoja aliyesaini mahudhurio licha ya majina kuonesha walihudhuria, alidai kuwa hakumbuki kwa kuwa miaka mingi imepita.

Naye mtendaji wa kijiji hicho (Waisaka) licha ya kudai wakati ardhi hiyo inatolewa kwa mwekezaji hakuwepo, alikiri kuandika barua hiyo ya Agosti 3, mwaka huu akirejea muhtasari wa mkutano wa wananchi uliofanywa na Mulongo Mei mwaka huu kwamba, tatizo ni mipaka ya ardhi ya wananchi na aliyomilikishwa mwekezaji kutofahamika.

error: Content is protected !!