July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wananchi Ngara waonywa kutouza ardhi kiholela

Spread the love

 

WANANCHI wa Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera nchini Tanzania wametakiwa kuacha kuuza ardhi kiholela na kuepuka kulima kwenye vyanzo vya maji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera …(endelea).

Wito huo umetolewa hivi karibuni wakati wa mafunzo ya sheria ya ardhi kwa wananchi wa vijiji vya Mumilamila, Nyabihanga, Bugarama, Mukubu, Rwinyana na Muganza yaliyotolewa na maofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara na kufadhiliwa na Kampuni ya Tembo Nickel.

Akitoa mafunzo hayo, Ofisa Ardhi Wilaya ya Ngara, Cosmas Lubambura aliwataka wananchi hao kuacha tabia ya kuuza ardhi bila kufuata sheria, kwani “wakati mwingine mmekuwa mkiuza ardhi hata kwa wananchi wa nchi jirani jambo ambalo ni kinyume na sheria.”

Pia, aliwataka kuhakikisha wanafuata sheria pale wanapolazimika kuuza ardhi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mashaidi wanakuwa majirani na kwa waliooa washirikishe wake zao ili kuepuka migogoro.

Kwa upande wake, Atanasio Andrew ambaye ni ofisa mazingira wa halmashauri hiyo, aliwataka wananchi hao kuacha tabia ya kulima kwenye vyanzo vya maji, akisema shughuli za binadamu kwenye vyanzo vya maji zimeanza kupunguza wingi wa maji katika maeneo hayo.

Alisema baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo, wamekuwa na tabia ya kuchoma moto hovyo jambo ambalo ni hatari kwani wakati mwingine huathiri mazao ya watu wengine.

“Inatakiwa mtunze mazingira ili muweze kufaidika na fursa mbalimbali, wenzetu wa Tembo Nickel wanatambua na kuthamini mchango wa mazingira na ndio maana wameamua kudhamini mafunzo haya,” alisema Andrew na kuongeza:

“Shughuli za mgodi zikianza kweli mazingira yanaweza kuathiriwa kwa kiasi flani, lakini mpango wa kudhibiti madhara ya mazingira ulioandaliwa na mgodi na kupitisha na serikali utafuata, kuhahikisha madhara yana pungua au kumalizwa kabisa.”

Naye Basil Shio kutoka Kampuni ya RSK, ambayo imepewa kandarasi ya kufanya tathimini na kuhamisha watu na makazi ili kupisha mradi wa Tembo Nickel, wakati ukifika, alisema jukumu lao ni kujua shughuli za kiuchumi, kukagua mali, kufanya tathimini na kwa wananchi ambao nyumba zao zipo kwenye eneo la mradi watahamishiwa maeneo mbadala.

“Tutapita kuchukua taarifa za watu, ukubwa wa maeneo kwa mtu mmojammoja na kuandaa majedwali ya malipo kwa mujibu wa sheria kisha ndiyo uhamishaji watu na wakazi utafuata.

“Tutakaa sana na ninyi viongozi na pia wananchi wanaoguswa na mradi wote tutakaa nao, tuongee na kujibu yote mliyonayo,” alisema.

error: Content is protected !!