WANANCHI wa Kijiji cha Ishenta Kata ya Ndola katika halmashauri ya wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe wamelalamikia kukosekana kwa maji safi na salama katika Kijiji hicho chenye zaidi ya wananchi 1,000 kutokana na miundombinu ya mradi uliopo mkuchakaa. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).
Wananchi hao wametoa malalamiko Kwa mkuu wa wilaya hiyo Mhe.Farida Mgomi leo tarehe 31 Oktoba 2023 kijijini hapo wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi.
Justa Kabungo ambaye ni mmoja wa wananchi wa Kijiji hicho, amesema wanahangaika kutafuta maji kutokana na mradi ambao upo kijijini hapo miundombinu yake imechakaa na kupelekea kushindwa kukidhi mahitaji ya wananchi kupata maji.
“Sisi wanawake wa Kijiji cha Ishenta tunahangaika sana kupata maji tunaomba serikali ituonee huruma itutue ndoo kichwani lengo likiwa ni kutuondolea adha wamama kuachana na matumizi ya maji ya kwenye visima ambayo si salama kwenye matumizi,” amesema Kabungo.
Elizabeth Mwampashi naye amesema katika msimu huu wa kiangazi wanahangaika kupata maji hususani wazee ambao hulazimisha kujitwisha ndoo za maji na kutembea umbali mrefu hali inayowalazimu kutumia maji ambayo si salama.
Akijibu kero za wananchi Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Arabi Namtaka amesema ili kutatua changamoto hiyo kijiji hicho kimewekwa kwenye mpango wa mwaka wa fedha 2024/ 2025.
Amesema mpango huo umelenga kupeleka mradi mkubwa wa maji ambao utatatua adha ya maji wanayokumbana nayo wananchi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi amewahakikishia wananchi hao kuwa serikali itahakikisha inamaliza changamoto hiyo kwani lengo la serikali ni kumtua mama ndoo kichwani.
Amesema pindi watakavyopewa mradi huo wanatakiwa kuwa walinzi ili udumu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibezya katika kata hiyo wakati wa mkutano wa hadhara, Mgomi amewaomba wananchi hao kulinda miundombinu ya mradi wa maji ambao umejengwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya Sh 600 milioni.
Leave a comment