Thursday , 25 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Wanakijiji Singida walia na mgodi
Habari MchanganyikoTangulizi

Wanakijiji Singida walia na mgodi

Spread the love

 

BAADHI ya wananchi wanaozunguka kampuni ya uchimbaji madini ya Ashanta kata ya Mang’onyi wilayani hapa wamedai kutonufaika na uwekezaji wake. Anaripoti Selemani Msuya, Ikungi … (endelea).

Wananchi hao walitoa malalamiko yao wakizungumza na Raia Mwema kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Mwau, Mang’onyi na Mlumbi vinavyozungukwa na mgodi huo.

Mkazi wa Mwau, Sabino Agustino, alisema mgodi huo wenye zaidi ya miaka 18 ya uwekezaji kwenye kata ya Mang’onyi haujanufaisha wananchi hasa vijana.

Alisema utaratibu wa kutoa ajira kwenye mgodi huo, umejikita kwenye itikadi za kichama, ambapo asilimia kubwa ya wanaopata kazi ni vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jambo ambalo si haki.

“Sisi tunataka wawekezaji, lakini mwekezaji anayeweza kuleta maendeleo kwetu, hii Ashanta tunaona haina faida kwetu, kwani wapo wananchi wanaumizwa na uwepo wake, mimi mdogo wangu amekutana na hayo madhila, hii si sawa, lakini pia mgodi huu haujatekeleza miradi ya kijamii (CSR) kwa kiwango kizuri,” alisema.

Agustino alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan awasaidie kupata eneo la kuchimba madini, ili kufaidika na rasilimali madini inayowazunguka.

“Rais Samia ameonesha nia ya kutaka kila Mtanzania anufaike na rasilimali za nchi, tunamwomba atusaidie tupate eneo la kuchimba, sisi wakazi wa Mang’onyi,” alisema.

Joshua Said aliomba kipaumbele cha kutoa ajira kizingatie wazawa kulingana na mahitaji na si watu kutoka nje ya kata hiyo.

Said alisema  mgodi huo ulianza wakati anamaliza shule ya msingi mwaka 2005, ila vijana wamekuwa wanateseka kupata ajira, jambo ambalo si sawa kwa upande wao.

“Nimeomba kazi zaidi ya mara tatu sipati, lakini wanakuja wageni wanapewa kazi ambazo hata sisi tunaweza kufanya,” alisema.

Gerald Bruno wa kijiji cha Mang’onyi ujio wa kampuni hiyo bado haijanufaisha wanakijiji katika eneo la kazi, kwani asilimia kubwa wanaofanya kazi ni watu kutoka nje ya kata hiyo.

Bruno alisema pia kuna madai kuwa wanaopata kazi ni makada wa CCM, hivyo aliomba changamoto hiyo ipewa ufumbuzi

Aidha, alisema pamoja na changamoto zilizopo, yapo ambayo yalifanywa na mgodi kama kujenga zahanati, madarasa, maji na matundu ya vyoo, ila ameomba kasi iongozeke, ili kufikia eneo kubwa.

“Mimi nimefanya kazi zaidi ya miaka tisa pale, ni kweli uzalishaji ulikuwa haujaanza ila kwa sasa wanazalisha, natarajia kuona CSR inakuwa kubwa zaidi,” alisema.

Joshua Said, mkazi wa kijiji cha Mang’onyi

Mmoja wa wanavijiji aliyeomba jina lake lisitajwe kwenye gazeti, alisema kitendo cha Serikali kufumbia macho malalamiko hayo, kinajenga chuki kati ya wananchi na Serikali yao.

Alisema mchakato wa wananchi kupata ajira umegubikwa na dalili za rushwa, jambo linasababisha watoto wa kimasikini kukosa nafasi.

Akijibu malalamiko hayo, Mtendaji wa Kijiji cha Mwau, Jumanne Gwaya alisema Ashanta imefanya mambo makubwa tangu mwanzo.

“Hapa Mwau tumepata matundu 22 ya vyoo yenye thamani ya Sh milioni 27, barabara ya Mwau, shule za msingi na sekondari Mwau pia vijana wameajiriwa na wengine wanafanya kazi kama vibarua,” alisema.

Mtendaji alisema Mwau na Tupendane wamenufaika na Ashanta lakini haijaingia kwenye eneo la leseni ya kampuni, ila Mang’onyi, Mulumbi na Sambaru, ardhi zao zimenufaika kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’onyi, Elineema Seti alisema mradi huo umewezesha upatikanaji ajira kwa vijana wasio na utaalamu mkubwa.

Seti alisema mradi huo umeongeza uhusiano mwema baina ya vijiji na kampuni, hivyo kuomba wananchi waudumishe.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlumbi, Issa Hamisi aliitaka kampuni kulipa fidia wananchi wanaohusika ili kuondoa manung’uniko.

Alisema Mlumbi imepata miradi michache ya maendeleo, hivyo kuomba fedha za CSR ili kutekeleza miradi mingine.

“Hapa Mlumbi tumepata CSR, bado mahitaji ni makubwa, hivyo tunaomba waongeze nguvu, tunahitaji maji, barabara, zahanati na shule, hili la ajira kwa misingi ya vyama siwezi kulizungumzia, kwani sijaona, kinachofanyika ni kuangalia sifa,” alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi

Akijibu kuhusu hoja ya Serikali kuwa na hisa Ashanta, Ofisa Madini Mkazi, Chone Malembo alisema kwa sasa kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia 100 na wawekezaji, lakini Serikali iko mbioni kupata asilimia 16 ya umiliki.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi, Ally Mwanga alisema ujio wa Ashanta umekuwa na neema kwa vijiji vitano, vinavyozunguka mgodi.

Mwanga alisema mgodi huo umeajiri wazawa wa Ikungi kipaumbele kikiwa ni wananchi wa Mang’onyi na kuna upendeleo au itikadi za vyama, si kweli.

“Ashanta walianza kutoa CSR kabla ya kuzalisha na sasa wameanza na mwaka huu tunatarajia kupata zaidi ya Sh milioni 270 kwa mwaka wa fedha 2023/24 na zitatumika katika vijiji husika,” alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi alisema mgodi huo ilianza mwaka 2005 kwa kufanya usanifu, ili kutambua maeneo yenye madini na mwaka 2017 walitambua maeneo na kulipa fidia takribani Sh bilioni 2, kujenga nyumba 16 na Msikiti.

Pia alisema kabla ya kuanza uzalishaji, walitoa CSR zaidi ya Sh bilioni moja na kwa mwaka huu fedha watoa zaidi ya Sh milioni 270.

“Hadi Machi mwaka huu, inadaiwa wamepata kilo 140 ya dhahabu ambapo Halmashauri ya Ikungi itapata zaidi ya Sh milioni 90, ikiwa ni mrabaha wa miezi mitatu. Ila pia kampuni zinazofanya kazi na Ashanta zimelipa Sh milioni 15,” alisema.

Aliongeza kuwa Ashanta imeajiri zaidi ya vijana wa kitanzania 350, hivyo kutoa rai kwa wananchi kuacha kupotosha kwa kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu mgodi huo.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema katika kuweka mazingira rafiki, wanatarajia kupima vijiji vyote vinavyozunguka mgodi huo.

Gazeti hili lilifika Ashanta na kukutana na Meneja Uhusiano, Elisante Mkumbo ili kujibu baadhi ya maswali akaomba atumiwe maswali, jambo linalofanyika, lakini hadi gazeti linakwenda mitamboni, hakuwa amejibu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!