August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanakijiji Dodoma wajifungulia vichakani

Mhe. Anthony Mavunde (MB), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu

Spread the love

WAKAZI wa kijiji cha Zepisa kata ya Hombolo Bwawani katika Manispaa ya Dodoma, wameiomba Serikali iwasaidie waweze kupata Zahanati iliyo karibu na makazi yao ili kuepukana na fedheha ya wanawake kujifungulia maeneo ya porini, anaandika Dany Tibason.

Wakizungumza na mtandao wa MwanaHALISI Online katika kijiji hicho ambacho kipo umbali wa Kilomita 50 kutoka katikati  ya mji wa Dodoma walisema wamekuwa wakijifungulia porini kutokana na umbali wa zaidi ya Kilomita 10 kwenda katika zahanati ya Hombolo Bwawani.

Evalina  Lugolein ambaye ni mkunga wa jadi amesema mpaka sasa amezalisha zaidi ya wanawake 800 kienyeji kutokana na kukosekana kwa zahanati katika kijiji hicho.

Amesema jina lake lipo katika zahanati ya Hombolo Bwawani kutokana na kina mama wote wanaojisikia uchungu katika kijiji cha Zepisa kwenda nyumbani kwake kwa lengo la kujifungua na kuwasindikiza Hombolo Bwawani.

“Kuna siku nilimsindikiza mama mmoja tukiwa porini usiku wa saa 6 akajisikia uchungu, dereva boda boda akakimbia nikabaki naye mimi tu, mara nikasikia sauti ya fisi niliogopa sana,” amesimulia.

Kwa upande wake Amina Matonya ambaye ni mkazi wa eneo hilo amesema wanawake wamekuwa wakijifungulia katika majani tu kutokana na kushikwa na uchungu wakiwa njiani wakielekea katika Zahanati.

“Tupo Manispaa kama hichi kijiji hawakitaki waseme tu, kuliko kutususa kiasi hiki. Sisi wamama jamani tunateseka, mwandishi tusaidie,” amesema.

Adovic Joseph amesema kutokana na umbali wa zahanati tayari amepoteza watoto wawili kutokana baada ya kukosa huduma ya haraka aliposhikwa na uchungu.

“Nina mtoto mmoja. Huyu ilibidi nilivyofikisha miezi 7 niende kwa ndugu zangu Dodoma ila hapo awali nilipoteza watoto mara mbili tena nikiwa porini kutokana na umbali wa zahanati,” amesema

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Justin Chilingo amesema kijiji hicho kimetelekezwa na serikali kwani ilijengwa zahanati na ambayo liliwekwa jamvi tu.

Daudi Kamunya, kaimu afisa mtendaji wa kata ya Hombolo Bwawani, alisema katika kijiji hicho kuna Kaya 1224 zenye wakazi zaidi ya 7,000 lakini wamekuwa wakiishi  maisha ya taabu kutokana na serikali kukitekeleza.

Godwin Kunambi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodomaakizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu amesema suala hilo linashughulikiwa huu Antony Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini (CCM) akiahidi kulishughulikia suala hilo.

error: Content is protected !!