June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanajeshi wawili wa Tanzania wauawa DR Congo

Wanajeshi wa Jeshi ya DR Congo wakiwa kwenye kambi ya waasi wa ADF

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon amelaani vikali shambulizi la kundi la waasi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambalo limeuwa wanajeshi wawili wa umoja huo wanatoka Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW), shambulizi hilo lilifanywa Jumanne jioni katika kijiji cha Kisiki, umbali wa kilometa 38 Kaskazini mwa mji wa Beni. Mbali na wanajeshi wawili waliouawa na 13 ambao walijeruhiwa, wengine wapatao wanne hawajulikani walipo.

Hata hivyo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), halikuwa tayari kukubali au kukanusha taarifa hizo, badala yake, msemaji wa jeshi hilo, Meja Joseph Massanja ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa “nasi tumezisikia taarifa hizo, hivyo ngoja tujipange ili tuwe kwenye nafasi nzuri ya kutoa taarifa iliyokamilika. Naomba nipewe muda hadi kesho.” 

Wanajeshi wa Tanzania ambao ni sehemu ya kikosi maalumu cha kuingilia kati, walikuwa wakifanya doria walipofanyiwa shambulizi hilo na watu wanaoaminika kuwa waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda. 

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema katibu huyo amesikitishwa sana na shambulizi hilo, na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea na juhudi zake za kuhakikisha usalama wa wakazi wa Mashariki mwa Congo wanaokabiliwa na vitisho vya waasi.

Shambulizi hilo lilikuwa la pili kufanywa dhidi ya Umoja wa Mataifa nchni Congo katika muda wa saa 48, kwani siku moja kabla, helikopta iliyokuwa imembeba Mkuu wa kijeshi wa ujumbe wa umoja huo nchini humo, MONUSCO, ilishambuliwa na watu ambao bado hawajatambuliwa.

Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler amesema hawataendelea kuvumilia mashambulizi hayo ya mara kwa mara dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Beni, na kuongeza kuwa MONUSCO itafanya operesheni kali dhidi ya waasi.

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo liliripoti jana kwamba liliwauwa waasi 16 wa ADF, katika mapambano makali yaliyofanyika eneo hilo mwishoni mwa juma lililopita. Jeshi hilo lilianzisha operesheni iliyoitwa Sukola mwaka jana, kwa azma ya kuwatokomeza waasi hao ambao wanashutumiwa kuwauwa watu 300 katika vijiji vilivyo karibu na mji wa Beni kati ya Oktoba na Desemba. 

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vililiunga mkono jeshi la Congo katika operesheni hiyo. Eneo la Mashariki mwa Congo limekuwa likikabiliwa na misukosuko kutokana na makundi mengi ya waasi, ADF ikiwa miongoni mwa makundi hayo, tangu kutokea kwa mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994.

MONUSCO ndio ujumbe mkubwa zaidi wa amani wa Umoja wa Mataifa kwa wakati huu, na unakihusisha kikosi maalumu chenye majukumu ya kipekee ya kuwashambulia waasi. Umoja huo umesema kuwa hadi 31 Machi mwaka huu, waajeshi wake 86 wamekufa nchini Congo, wengi kutokana na maradhi na ajali.

error: Content is protected !!