July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanaharakati wampopoa Magufuli

Spread the love

RAIS John Magufuli hajakidhi matakwa ya wanawake wa nchi hii licha ya kuahidi kufanya hivyo kwenye kampenzi zake za urais mwaka jana, anaandika Happyness Lidwino.

Wanaoonesha kutoridhishwa na namna Rais Magufuli alivyowapa nafasi wanawake kwenye uteuzi wa nafasi mbalimbali nchini ni wanaharakati wa kutetea usawa wa kijinsia Tanzania ambao wamekutana leo jijini Dar es Salaam kujadili siku 100 za uongozi wake.

Wamesema kwamba, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilieleza kuzingatia usawa kwa asilimia 50 jambo ambalo Rais Magufuli hajalizingatia na kwamba amefufua mfumo wa zamani ambao ni kandamizi.

Akizungumzia siku 100 za Rais Magufuli, Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi wa TGNP Mtandao amesema, wanaharakati wamesikitishwa na uteuzi wa Baraza la Mawaziri ambalo halikuzingatia usawa wa kijinsia.

“Kwa ujumla Rais Magufuli hakuzingatia usawa wa kijinsia. Mfano kati ya mawaziri na manaibu mawaziri 35, wanawake ni tisa pekee sawa na asilimia 25.7 huku wanaume wakiwa 26 sawa na asilimia 74.28.” amesema na kuongeza;

“Makatibu wakuu na manaibu wananwake walioteuliwa ni 10 pekee sawa na asilimia 20 tu huku wanaume wakishikilia asilimia 80. Siku 100 hazitoshi kumhukumu ila tunaangali muamko wake wa kuwapigania wanawake bado uko nyuma.”

Akizungumzia suala la elimu kwa upande wa watoto wa kike Dk. Alexander Makulilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala amesema, japo amejitahidi kutekeleza ahadi ya elimu bure lakini bado hajaweka wazi mikakati ya kuwasaidia watoto wa kike katika masomo yao.

Amesema, anatakiwa kuweka mfumo utakaowasaidia watoto wa kike katika masomo yao ili kutimiza ndoto zao. “Japo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imebainisha usawa wa kijinsia kwamba itakuwa ni 50 kwa 50 lakini bado hajaanza kutekeleza. Tulitegemea ndani ya siku 100 angeweka mikakati ya kumsaidia mototo wa kike.”

Amesema, kuna haja ya serikali kuboresha mifumo ya uongozi kuanzia ngazi za chini hadi juu pia kuwa na katiba mpya itakayozingatia jinsia na kuwashirikisha wanawake.

Wanaharakati hao wametoa rai kwa Rais Magufuli kuzingatia usawa wa kijinsia katika teuzi zijazo na pia mawaziri na viongozi wengine wazingatia usawa wa jinsia katika shughuli zao wanazofanya kila siku ili kuhakikisha mahitaji ya wanawake, walemavu, watoto wazee na vijana yanazingatiwa.

error: Content is protected !!