December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanahabari watakiwa kuibua masuala yanayowainua wanawake katika uongozi

Waandishi wa Habari

Spread the love

 

WAANDISHI wa habari nchini Tanzania, wametakiwa kutumia kalamu zao katika kuibua masuala yanayowainua wanawake katika uongozi wa nyanja mbalimbali serikalini na kwenye taasisi binafsi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa na wadau mbalimbali katika mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kuhusu usawa wa kijinsia katika uongozi, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Internews na kufanyika mtandaoni tarehe 16 hadi 17 Novemba 2022.

Afisa Uchechemuzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Florence Majani, akiwasilisha mada kuhusu namna gani vyombo vya habari vitachochea uongozi wa wanawake, alisema njia pekee ya kufanikisha suala hilo ni kwa waandishi wa habari kuibua mafanikio yanayofanywa na viongozi wa kike, ili kuondoa dhana potofu kwamba hawawezi.

“Hatukuwahi kufikiria kama ipo siku Tanzania tutakuwa na kiongozi mkubwa mwanamke, lakini leo hii tuna Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan na anafanya vizuri sasa hivi anaingia mwaka wa tatu. Wizara ya ulinzi tulikuwa tunadhani haiwezi ongozwa na mwanamke lakini alikuwepo Dk. Stegomena Tax na alifanya vizuri,” alisema Florence na kuongeza:

“Hii imewezekana kwa sababu ya vyombo vya habari kuandika mafanikio ya wanawake waliopata nafasi za uongozi. Vyombo vya habari tunafananisha na taa iliyofunikwa na kikapu, kazi yake ni kufunua kapu na kuacha taa ifanye kazi yake ambayo ni kuibua mafanikio ya wanawake, kuhamasisha wanawakje kushindana katika nafasi za uongozi.”

Mhariri wa TBC 1, Anna Mwasyoke, akitoa mada kuhusu namna ya kuchochea usawa wa kijinsia ndani ya vyumba vya habari, aliwataka wamiliki na wahariri wa vyombo hivyo kuhakikisha usawa unakuwepo kati ya wanawake na wanaume, katika uendeshaji wake, kuanzia kwenye uongozi, uandaaji maudhui hadi uwasilishaji wake kwa umma kupitia uchapishaji au utangazaji.

Mhariri wa Pemba Today kutoka visiwani Zanzibar, Haji Mohamed alisema “wajibu wa vyombo vya habari inatakiwa ufanyike ipasavyo ili kufikia usawa wa jinsia, lazima usawa uanzie katika uongozi kama mhariri ni mwanaume msaidizi wake awe mwanamke. Lakini pia vyumba vya habari viamini vyanzo vya habari vinavyotoka kwa wanawake ili kuwajengea ujasiri wa kuzungumzia masuala yao.”

Akifunga mafunzo hayo, Mtaalamu wa Masuala ya Vyombo vya Habari wa Internews, Alakok Mayombo, amewataka washiriki kutumia vyema mafunzo hayo katika utekelezaji wao wa majukumu, ili kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika uongozi unaongezeka.

error: Content is protected !!