WAKULIMA wa bonde la mpunga la Mgongola lililopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wameiomba serikali kuwapatia hatimiliki za mashamba yao ili waweze kuyaendeleza bila kubughudhiwa na wafugaji. Anaripoti Christina Haule, Mvomero … (endelea).
Ombi hilo lilitolewa jana na mshiriki wa mdahalo wa amani na elimu shirikishi kwa umma juu ya utatuzi migogoro ya ardhi kwa sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999 ulioandaliwa na Chama cha Waandishi Habari mkoani Morogoro (MPC) kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society (FCS).
Mdahalo huo ulifanyika kwa wananchi wa kata ya Mvomero, Hembeti na Dakawa ukihusisha viongozi wa vijiji na wajumbe wa mabaraza ya usuluhishi.
Wakulima hao akiwemo Chamhingo Kibamba walisema wanakabiliwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yao huku serikali kupitia MPC kuwapatia hati wazitumie kupata mkopo na kuendesha kilimo cha umwagiliaji.
Chamhingo alisema kuwa upatikanaji wa hati utawafanya kupata hela za pamoja kutoka taasisi za fedha na hivyo kuwawezesha kujenga miundombinu ya umwagiliaji wa zao la mpunga.
“Hata mtu akiwa na fedha mwenyewe hawezi kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwa sababu wafugaji wataingiza ng’ombe na kuharibu sababu wanajiona kuwa wao ndio wenye mashamba na kutuamrisha hata kutoa mazao haraka ili waingize ng’ombe kwa ajili ya malisho,” alisema Kibamba.
Wenyeviti wa mabaraza ya ardhi ya kata hizo za Hembeti, Mvomero na Dakawa waliishukuru MPC kwa elimu hiyo waliyoanza kuitoa miezi kadhaa iliyopita kwani imeweza kuwasaidia kupunguza kesi za migogoro ya ardhi katika mabaraza ya ardhi kwenye maeneo yao.
Mwenyekiti wa baraza la ardhi kata ya Hembeti Hassan Songoro amesema, migogoro ya ardhi imepungua kutoa kesi 16 mwaka 2016 hadi kufikia kesi 8 mwaka 2017.
Leave a comment