December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wanafunzi wapya Chuo cha Mwalimu Nyerere wakaribishwa kwa ujumbe

Spread the love

 

MKUU wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, Prof Shadrack Mwakalila amewataka wanafunzi wa chuo hicho kujiepusha na masuala ya kisiasa na wajielekeze katika mambo ya msingi yanayohusiana na taaluma ili kupata maarifa bora yatakayowasaidia katika maisha yao na taifa kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema hayo leo Jumatano, tarehe 24 Novemba 2021, wakati akiwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo hicho na kusisitiza chuo hicho hakiruhusu itikadi za siasa.

Profesa Mwakalila amesema, ndiyo maana wakati wa udahili hakuna mwanafunzi aliyeulizwa chama anachotoka. Pia, amewaasa wafanyakazi wote wa chuo hicho kutoa huduma bora kwa wanafunzi ili waweze kusoma na kupata maarifa bora.

“Ili uweze kupata maarifa bora lazima mwanafunzi usome kwa juhudi na maarifa, uwe muadilifu na mzalendo hii itakusaidia wewe na Taifa, jiepusheni na makundi ya uchochezi na mzingatie zaidi masomo pamoja na kujiepusha na udanganyifu wowote kwenye mitihani,” amesema Prof. Mwakalila.

Aidha, Prof. Mwakalila amewataka watumishi wa chuo hicho kutoa huduma zilizo bora kwa wanafunzi wote ili kujenga Taifa lenye wataalamu wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mkuu huyo wa chuo ameahidi uongozi wa chuo utahakikisha unaboresha mazingira ya kujifunzia ili kila mwanafunzi aweze kupata maarifa bora katika mazingira bora.

error: Content is protected !!