November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wanafunzi walilia madarasa Mtwara, Silinde awajibu

Spread the love

 

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Mpowora, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, wameiomba Serikali kuwajengea madarasa kwani yaliyopo ni mabovu na yanahatarisha usalama wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Masasi … (endelea). 

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1982, ina madarasa chakavu huku ikiwa haina choo cha walimu, hali inayowafanya walimu na wanafunzi kutumia choo kimoja.

Ombi la wanafunzi hao, wamelitoa mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde, aliyefika shuleni hapo kukagua na kutoa maagizo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Japhet Anord alisema “naomba Serikali isaidie madarasa yetu, mbao zimeliwa na mchwa, shuleni madirisha hakuna, ninachoomba Serikali kama ina visenti kidogo ije kutuboreshea shule yetu.”

Mwanafunzi mwingine, Shamira Bushiri alisema “Serikali ije kutusaidia shule yetu kwani haina milango na muda wowote inaweza kubomoka, mvua ikinyesha maji yanaingia darasani.”

Baada ya kukagua mazingira ya shule hiyo na kusikiliza maombi ya wanafunzi hayo, naibu waziri, Silinde alisema “kwa kweli, kutoka katika sakafu ya moyo wangu, yale madarasa yamechoka sana na ni mabovu kwelikweli.”

Silinde amesema, kwa hatua ya dharura, Ofisi ya Tamisemi itaingiza Sh.40 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili au matatu “na hii ni nje ya bajeti, tutaingiza kwenye mpango wa bajeti, ili kuweza kusaidia mazingira ya hapa.”

Awali, Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe alisema, shule hiyo ni chakavu sawa na shule 29 zenye mazingira kama hayo hivyo, “nikuombe wewe (Silinde) na Rais (John Magufuli), ili kusaidia hili.”

error: Content is protected !!