September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wanafunzi Vyuo Vikuu ‘wanakula nyasi?’

Spread the love

LEO ni siku ya tatu mfululizo, tangu wanafunzi wa vyuo vikuu kote nchini kuanza mafunzo kwa vitendo (practical trainings) bila Serikali kuwapatia fedha za kujikimu ikiwemo na nauli ya kuwawezesha kufika katika vituo vyao, anaandika Charles William.

Kitendo hiki ni kinyume na mkataba baina ya wanafunzi hao na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu hapa nchini (HESLB) lakini pia ni kinyume na ahadi ya serikali iliyotolewa wiki mbili zilizopita kuwa wanafunzi hao wangepewa fedha za kujikimu kwaajili ya mafunzo kwa vitendo kabla ya 8 Agosti mwaka huu.

Katika mkutano na vyombo vya habari, wiki mbili zilizopita Prof. Joyce Ndalichako Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alidai kuwa serikali imeshindwa kuwapa wanafunzi fedha za mafunzo kwa vitendo kutokana na zoezi la kuhakiki wanafunzi hewa na kwamba imesogeza mbele kuanza kwa zoezi hilo la kitaaluma kutoka 25 Julai mwaka huu mpaka 08 Agosti mwaka huu.

Prof. Ndalichako aliahidi kuwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu kote nchini ambao ni wanufaika wa mikopo wangepewa fedha hizo kabla ya Agosti 08 mwaka huu, jambo ambalo limeshindikana mpaka sasa huku waziri huyo akishindwa kutoa ufafanuzi juu ya wanafunzi kuanza mafunzo kwa vitendo bila fedha za kujikimu jambo linalowapa wakati mgumu.

Tangazo lililotolewa 4 Agosti mwaka huu na utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia kwa Profesa Florens Luoga ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia masuala ya taaluma limewataka wanafunzi wote wa Chuo hicho kuripoti katika vituo vyao vya mafunzo kwa vitendo huku likidokeza kuwa serikali itawalipa fedha zao za kujikimu kwa awamu (installments).

Agizo hilo limewafanya wanafunzi hao kuanza mafunzo kwa vitendo huku Serikali yao ya Wanafunzi (DARUSO) ikitoa matamko mawili ya kujikanganya ambapo katika tamko lililotolewa kwa wanahabari na Erasmi Leon 06 Agosti mwaka huu aliwasihi wanafunzi hao kugomea kuanza mafunzo kwa vitendo bila kupata fedha zao lakini siku moja baadaye alitoa tangazo lingine akiwataka wanafunzi hao kuanza zoezi la mafunzo kwa vitendo bila kubainisha ni lini watapokea fedha zao.

Prof. Ndalichako amenukuliwa hivi karibuni akisema Serikali tayari imeshaidhinisha malipo hayo na kwamba mchakato wa malipo katika akaunti za wanafunzi upo mikononi mwa bodi ya mikopo, hata hivyo Mwanahalisi online ilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa HESLB hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na kuomba mwandishi amtafute ofisa mawasiliano wa HESLB Cosmas Mwaisobwa ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana.

Hata hivyo taarifa zilizotolewa na mmoja wa maofisa wa bodi ya mikopo ambaye hakutaka kutajwa kwa madai kuwa yeye si msemaji zinasema kuwa serikali ipo hoi kifedha ndiyo maana imechelewesha kutoa fedha kwa bodi hiyo ili ziweze kuwafikia wanafunzi.

“Ndugu yangu sisi HESLB tunasingiziwa tu, serikali haina fedha uhakiki wa wanafunzi hewa umeshamalizika muda mrefu lakini wakatuambia hawana fedha za kuwapa wanafunzi na inabidi walipwe nusu nusu tofauti na utaratibu wa miaka mingine ambayo tulikuwa tunawalipa fedha zote, sasa hivi ndiyo tupo kwenye mchakato wa kuvipelekea vyuo vyote fedha hizo,” amedokeza.

Hii siyo mara ya kwanza kwa serikali kuwalazimisha wanafunzi kwenda katika mafunzo kwa vitendo bila kuwapa fedha zao za kujikimu kama mikataba yao na bodi ya mikopo inavyoelekeza.

Mwaka 2014 wanafunzi hao waliwahi kucheleweshewa malipo hayo kwa zaidi ya mwezi mmoja huku serikali ikidai kutokuwa na fedha hata hivyo hali hii haikutarajiwa kujitokeza katika wakati huu kutokana na serikali kujinadi mara kwa mara kuwa imepandisha ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa 800 bilioni kwa mwezi mpaka kufikia zaidi ya 1.2 trilioni.

Itakumbukwa kuwa kutochelewesha mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu ilikuwa ni miongoni mwa ahadi za mara kwa mara za Rais John Magufuli wakati akiwania nafasi ya urais mwishoni mwa mwaka jana na zaidi ya yote alijiapiza kuwa angemfukuza kazini mtumishi yoyote wa umma ambaye angesababisha kucheleweshwa kwa fedha hizo za wanafunzi wa vyuo vikuu.

Hata hivyo hali imekuwa tofauti. Hakuna mtumishi wa serikali aliyefukuzwa. Kilichoahidiwa na Rais Magufuli kimeshindikana, hata ahadi ya Prof. Ndalichako ya kuwalipa wanafunzi kabla ya 08 Agosti mwaka huu imeshindika lakini pia hata ahadi ya HESLB kuwalipa wanafunzi hao nusu ya fedha kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo imeshindikana.

Wanafunzi wanasisitizwa kwenda katika vituo vyao vya mafunzo kwa vitendo huku wakiwa hawana fedha za kujikimu.

Nauli wanatoa wapi? Pengine wanatembea kwa miguu na kuomba lifti. Wanakula nini na kwa gharama za nani? Pengine wanashinda njaa na kuomba wenyeji wao katika vituo vyao wawape msaada au wanakula ‘nyasi’ kama ilivyopata kusemwa huko nyuma.

error: Content is protected !!