WANAFUNZI wa Kidato cha Nne wa mchepuo wa sayansi katika Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Mivumoni – Kindondoni, Mtambani jijini Dar es Salaam, wameunda kifaa chenye uwezo wa kutambua viashiria vya moto. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).
Leo tarehe 22 Agosti 2019, wanafunzi hao wameeleza namna walivyounda kifaa hicho kinachofahamika kwa jina la Simple Fire Alarm pamoja na matumizi yake.
Ibrahim Juma, mwanafunzi wa shule hiyo ndiye alitoa wazo wa utengenezwaji wa kifaa hicho na kisha kushirikisha darasa lake.
Kwa kushirikiana na wenzake Ibrahim amesema, wameunda kifaa hicho baada ya kuona majanga ya moto yamekithiri na kuharibu mali na hata kupoteza maisha ya watu.
“Tumeunda kifaa hiki baada ya kuona athari za ajali za moto. kwa msaada wa uongozi wa shule, wametununulia vifaa na sisi tukaunda,” amesema Juma.
Akielezea namna kifaa hicho kinavyofanya kazi, Hafswaa Fadhil ambaye pia ni mwanafunzi wa shule hiyo, amesema kifaa hicho kina uwezo wa kutambua ongezeko la joto lisilo la kawaida.
“Endapo jengo husika kuna moto unawake, kifaa hiki huanza kutambua ongezeko la joto,” amesema Hafswaa.
Akifafanua zaidi utendaji kazi wa Simple Fire Alarm, Bilqis Njama, mwanafunsi wa masomo ya sayansi kwenye shule hiyo amesema, baada ya kifaa hicho kutambua joto lisilo la kawaida, huanza kutoa muito wa dharura ‘alarm’.
“Pindi moto unapowaka na joto lisilo la kawaida kuongezeka, kifaa hiki huanza kutoa mlio wa hatari. Mlio huo utawawezesha wahusika walio karibu na jengo kujua kwamba kuna hali ya hatari na kuanza taratibu za kuzuia ajali ya moto,” amesema Njama.
Mwalimu wa shule hiyo, Barick Mwalongo amesema wanafunzi hao wamebuni kifaa hicho baada ya kufundishwa mada ya elekroniki katika somo la Fizikia, ambapo uongozi wa shule hiyo uliwawezesha kupata vifaa vya kuunda kifaa hicho.
“Wanafunzi hawa walifundishwa mada ya elektroniki, baada ya kuelewa somo wakaamua kuunda kifaa hicho. Sisi tuliwawezesha kupata vifaa walivyovihitaji na kufanikiwa kukamilisha zoezi hilo,” amesema Mwalongo.
Leave a comment