August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanafunzi hewa watubu walimu Mwanza

Wanafunzi wa shule ya msingi

Spread the love

CHAMA cha Walimu (CWT) na Umoja wa Wakuu wa Shule za Msingi katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wamesema kuwa, wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kisheria ili kumfikisha mahakamani Kiomoni Kibamba, mkurugenzi wa jiji hilo, anaandika Moses Mseti.

Ni kutokana na kumpinga hatua ya Kibamba kuwasisimamisha na kuwavua madaraka wakuu wa Shule za Msingi 62 kwa madai kwamba, walisajili wanafunzi hewa katika shule zao kwa lengo la kujipatia fedha.

Msimamo huo umetolewa leo na Asha Juma, Katibu wa Umoja wa Wakuu wa Shule Wilaya ya Nyamagana mbele ya waandishi wa habari na wakuu wa shule hizo waliosimamishwa na kuvuliwa madaraka.

Asha amesema kuwa, mkurugenzi wa jiji hilo alichukua uamzi wa kukurupuka huku akidai, hana mamlaka ya kumfukuza mwalimu yeyote.

Hata hivyo amesema, wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu na kwamba muda wowote kuanzia sasa watamfikisha kortini ili kujibu tuhama za kuwafukuza walimu hao bila kufuata taratibu.

“Kama sio maamzi ya kukurupuka ni kitu gani, haiwezekani. Kuna walimu wametangulia mbele za haki na wengine sasa hivi wameteuliwa kuwa viongozi ngazi tofauti serikalini lakini na wao wamejumuishwa humo.

“Kuna mwalimu January Sigareti ameteuliwa kuwa DC (Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Tanga), Abas Mohamed (amestaafu), Nasoro Rashid (amefariki) na Jummane Nyanda ambaye alipata ofa kuwa Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu Buhingwe, Geita na wao wamo, kama sio kukurupuka ni nini?” amehoji.

Amesema kuwa, mkurugenzi huyo alishindwa kufanya uchunguzi wa kina na kuanza kuchukua hatua ikiwemo kitendo cha kuorodhesha walimu waliofariki muda mrefu kwamba wapo katika vituo vyao vya kazi.

Hata hivyo mkurugenzi Kibamba alipotafutwa na mtandao huu kuzungumzia suala hilo, alidai hawezi kutengua uamzi wake na kwamba, vyombo vyake vilifanya uchunguzi na kupata ukweli wa walimu kusajili wanafunzi hao.

error: Content is protected !!